Mourinho amnunulia mchezaji wake wa AS Roma zawadi ya viatu baada ya kufunga mabao mawili dhidi ya Genoa ligini

Mourinho amnunulia mchezaji wake wa AS Roma zawadi ya viatu baada ya kufunga mabao mawili dhidi ya Genoa ligini

Na MASHIRIKA

KOCHA Jose Mourinho wa AS Roma alimnunulia Felix Afena-Gyan jozi ya njumu za kuchezea soka baada ya fowadi huyo chipukizi raia wa Ghana kufunga mabao yake ya kwanza katika Ligi Kuu ya Italia (Serie A).

Afena-Gyan, 18, alitokea benchi katika dakika ya 75 na kusaidia Roma kusajili ushindi wa 2-0 dhidi ya Genoa. Sogora huyo alifunga bao la kwanza katika dakika ya 82 baada ya kukamilisha krosi ya Henrikh Mkhitaryan na akamkimbilia Mourinho pembezoni mwa uwanja.

“Nilimwahidi jozi ya viatu vya kuchezea, daluga za euro 800 na alihakikisha kwamba amekuja kwangu baada ya kufunga bao ili nisihau ahadi niliyokuwa nimempa,” akasema Mourinho.

Afena-Gyan aliachilia kombora jingine mwishoni mwa kipindi cha pili na kuduwaza mashabiki uwanjani Stadio Luigi Ferraris. Ushindi huo uliwapaisha Roma hadi nafasi ya tano kwenye msimamo wa jedwali la Serie A.

Mourinho alitimiza ahadi yake na akampa sogora huyo zawadi yake mnamo Novemba 22, 2021. Afena-Gyan ambaye sasa anafuatiliwa pakuba na timu ya taifa ya Ghana, aliwajibishwa na Mourinho katika kikosi cha watu wazima kambini mwa Roma kwa mara ya kwanza mnamo Oktoba 27, 2021 dhidi ya Cagliari.

Aliletwa pia uwanjani katika kipindi cha pili dhidi ya AC Milan kabla ya kampeni za Ligi Kuu kupisha michuano ya kimataifa. Aliitwa na Ghana kambini mwao kwa ajili ya mechi za kufuzu kwa Kombe la Dunia 2022 dhidi ya Ethiopia na Afrika Kusini mwezi huu na akakataa ofa hiyo.

Kwingineko nchini Italia, kiungo wa Alfred Duncan wa Ghana alifunga bao la ufunguzi na kusaidia Fiorentina kushinda AC Milan 4-3 huku David Okereke wa Nigeria akifunga bao la pekee lililowapa Venezia ushindi wa 1-0 dhidi ya Bologna ugenini.

You can share this post!

Mkitunyima huduma za serikali, basi msituombe kura –...

Pigo Nigeria na Napoli baada ya mvamizi Osimhen kuvunjika...

T L