Michezo

Mourinho amvua Pogba unahodha

September 26th, 2018 1 min read

Na CECIL ODONGO

MKUFUNZI wa Manchester United Jose Mourinho amethibitisha kwamba kiungo Paul Pogba amepokonywa unaibu nahodha wa timu ingawa akapuuza kwamba kuna uhusiano baridi kati yake na mwanasoka huyo wa zamani wa Juventus ya Italia.

“Ukweli ni kwamba nimeafikia uamuzi wa kumpokonya Paul unahodha wa timu lakini si kwasababu hatuelewani naye, hakuna shida kati yetu. Mimi ndiye wa kuamua nani atakuwa nahodha na nani atakuwa mchezaji wa kawaida. Mimi ndiye kocha na huu ni uamuzi ambao si lazima niuelezee,” akasema Mourinho.

Pogba alikuwa nahodha wa Manchester United wakati wa mechi za ligi ya EPL dhidi ya Leicester City, Brighton and Hove Albion na katika mechi ya ligi ya Bara Uropa dhidi ya Young Boys,nahodha wa timu Antonio Valencia alipokosekana kikosini.

Hata hivyo Pogba hakuunga wala kukamilisha kikosi kilichobanduliwa nje ya kombe la Carabao na Derby County inayotiwa makali na Staa wa zamani Chelsea Frank Lampard.

Katika mechi hiyo iliyoishia sare ya 2-2 muda wa kawaida, difenda Phil Jones alikiingiza kitumbua cha Manchester United  mchangani baada ya kupoteza penalti na mechi ikaisha 8-7 kwa faida ya Derby County.