Michezo

Mourinho amweka Rodgers presha

July 20th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

FOWADI na nahodha Harry Kane alifunga mabao mawili na kusaidia Tottenham Hotspur kuwachabanga Leicester City 3-0 katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Julai 19, 2020.

Ni matokeo ambayo yaliendeleza presha zaidi kwa Leicester ambao kwa sasa wapo katika hatari ya kukosa nafasi ya kushiriki kipute cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu ujao iwapo Manchester United watakizamisha chombo cha West Ham United uwanjani Old Trafford mnamo Julai 22 na kuambulia sare ya aina yoyote dhidi ya Leicester uwanjani King Power mnamo Julai 26.

Kufuzu au kutofuzu kwa Leicester kwa kivumbi cha UEFA msimu ujao kutategemea jinsi Chelsea watakavyotoka na Liverpool na Wolves katika mechi mbili za mwisho. Chini ya kocha Brendan Rodgers, Leicester wameratibiwa kukamilisha kampeni za EPL msimu huu dhidi ya Man-United katika mechi ya kufa-kupona mnamo Julai 26 ugani King Power.

Chelsea ambao wamesakata jumla ya mechi 36 kutokana na 38 za msimu huu, kwa sasa wanashikilia nafasi ya tatu kwa alama 63, moja pekee kuliko Man-United na Leicester ambao walitawazwa mabingwa wa EPL mnamo 2015-16.

Kufikia sasa, Man-United wanashikilia nafasi ya tano jedwalini kwa alama 62 sawa na Leicester ambao wamesakata mchuano mmoja zaidi kuliko washindani wao hao wakuu katika vita vya kufuzukia fursa ya kukamilisha kampeni za msimu huu ndani ya mduara wa nne-bora na kujikatia tiketi ya kunogesha kipute cha UEFA muhula ujao.

James Justin alijifunga katika dakika ya sita na kuwapa Tottenham bao muhimu lililoamsha hamasa ya masogora wa kocha Jose Mourinho ambao waliongeza mabao mawili ya haraka kupitia kwa Kane kunako dakika ya 37 na 40 mtawalia.

Ingawa Leicester walipata nafasi nyingi za wazi, makali yao hayakumtikisa kipa Hugo Lloris aliyesalia imara langoni na kupangua makombora mazito aliyoelekezewa na Jamie Vardy, Ayoze Perez na Demarai Gray.

Ushindi kwa Tottenham ambao watafunga kampeni za msimu huu dhidi ya Crystal Palace uwanjani Selhurst Park mnamo Julai 26, kwa sasa uliwapaisha hadi nafasi ya sita kwenye msimamo wa jedwali kwa alama 58, mbili zaidi kuliko Wolves ambao walikuwa wenyeji wa Crystal Palace mnamo Julai 20 ugani Molineux.