Mourinho aongoza AS Roma kutandika Feyenoord na kutwaa taji la Europa Conference League

Mourinho aongoza AS Roma kutandika Feyenoord na kutwaa taji la Europa Conference League

Na MASHIRIKA

AS Roma walinyanyua taji lao la kwanza katika soka ya bara Ulaya kwa kutandika Feyenoord ya Uholanzi 1-0 katika fainali ya kipute kipya cha Europa Conference League iliyofanyika jijini Tirana, Albania mnamo Jumatano usiku.

Kwa hivyo, msimu wa kwanza wa kocha Jose Mourinho kambini mwa Roma ulikamilika kwa taji baada ya kiungo mvamizi Nicolo Zaniolo kupachika wavuni bao la pekee na la ushindi lililochangiwa na Gianluca Mancini katika dakika ya 32.

Mourinho ambaye pia anajivunia kushinda mataji ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA), Europa League na Uefa Cup, ndiye mkufunzi wa kwanza kuwahi kutwaa mataji yote makuu ya mashindano ya Uefa.

Kocha huyo raia wa Ureno alikashifiwa na kukosolewa pakubwa kikosi chake cha Roma kilipopepetwa kwa mabao 6-1 na Bodo/Glimt ya Norway katika mojawapo ya mechi za makundi ya Europa Conference League mnamo Oktoba 2021 nchini Norway.

Hata hivyo, ushindi dhidi ya Feyenoord uliendeleza rekodi nzuri ya Mourinho katika fainali za soka ya bara Ulaya ikizingatiwa kwamba sasa ameshinda fainali tano kati ya zote tano ambazo vikosi alivyowahi kunoa vikiwemo Chelsea na Manchester United vimenogesha.

“Hiki ni kipute ambacho tuliamini tuna uwezo wa kushinda tangu mwanzoni. Nilifahamu matarajio makuu kutoka kwa mashabiki, wachezaji na wasimamizi wa Roma pindi nilipokubali mikoba ya kikosi hiki. Wamekuwa wakihitaji kitu spesheli kama hiki na tumeanza kuandika historia,” akasema Mourinho ambaye pia amewahi kunoa Inter Milan, Real Madrid na Tottenham Hotspur.

Feyenoord walioanza kampeni zao za Europa Conference League lwa kufuzu kwa raundi za mchujo mnamo Julai, walipoteza fursa nzuri ya kusawazisha mwishoni mwa kipindi cha pili baada ya kipa Rui Patricio kupangua kombora la Tyrell Malacia na kushuhudia mpira ukibusu mwamba wa goli.

Taji hilo lilikuwa la kwanza kwa Mourinho kunyanyua tangu aongoze Man-United kujizolea kombe la Europa League mnamo 2017.

Beki Chris Smalling, 32, aliyekuwa sehemu ya kikosi kilichotegemewa na Man-United kwenye fainali hiyo dhidi ya Ajax jijini Stockholm, Uswidi miaka mitano iliyopita, alitamba zaidi kambini mwa Roma walionyanyua taji lao la kwanza tangu 2008.

Sogora mwingine aliyeridhisha zaidi kambini mwa Roma ni fowadi Tammy Abraham aliyesajiliwa kutoka Chelsea kwa Sh5.3 bilioni mnamo Agosti 2021.

Nyota huyo alikamilisha msimu wake wa kwanza akivalia jezi za Roma kwa mabao 27 katika mashindano yote muhula huu na kujipa matumaini makubwa ya kuwa sehemu ya kikosi cha Uingereza kitakachotegemewa na kocha Gareth Southgate katika fainali za Kombe la Dunia nchini Qatar mnamo Novemba-Disemba 2022.

MAFANIKIO YA MOURINHO KATIKA SOKA YA BARA ULAYA:

KLABU    MSIMU  TAJI

Porto      2002-03 Uefa Cup

Porto      2003-04 Klabu Bingwa Ulaya

Inter Milan    2009-10 Klabu Bingwa Ulaya

Man-United  2016-17 Europa League

Roma     2021-22 Europa Conference League

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Tetesi: Arsenal, Dortmund wamezea mate beki Okumu

Borussia Dortmund waajiri kocha Edin Terzic

T L