Michezo

Mourinho asema Spurs watampa beki Eric Dier kandarasi mpya

July 2nd, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

KOCHA Jose Mourinho wa Tottenham Hotspur amesema kikosi chake kitampa beki matata mzawa wa Uingereza, Eric Dier, 26, mkataba mpya baada ya kandarasi yake ya sasa kutamatika rasmi mwishoni mwa msimu ujao.

“Mwenyekiti wa Tottenham, Daniel Levy, ameniambia kwamba anamtaka Dier atie saini mkataba mpya. Dier amesema amefurahishwa na maisha yake kambini mwa Tottenham na atakuwa radhi kuchezea kikosi hiki kwa kipindi kirefu zaidi,” akasema Mourinho.

“Natumai kwamba wataafikiana hivi karibuni kwa sababu ninapanga kukisuka kikosi nitakachokitegemea kwa kampeni za msimu ujao,” akasema Mourinho.

Dier amewajibishwa kama beki wa kati, nafasi anayoipenda sana, katika mechi mbili zilizopita za Tottenham tangu kurejelewa upya kwa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) iliyosimamishwa mnamo Machi 13, 2020 kutokana na janga la corona.

Chini ya kocha Mauricio Pochettino ambaye alikuwa mtanguliza wa Mourinho, Dier aliwajibishwa sana kama kiungo mkabaji.

Dier aliingia katika sajili rasmi ya Tottenham mnamo 2014 kwa kima cha Sh560 milioni baada ya kuagana na Sporting Lisbon ya Ureno. Tangu wakati huo, amechezeshwa katika jumla ya mechi 171 na akafunga mabao 10.