Michezo

Mourinho guu moja tu kurudi kambi ya Real

August 6th, 2019 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

KUKOSA kwa kiungo Paul Pogba kuingia katika sajili rasmi ya Real Madrid msimu huu na jaribio la kumfurusha Gareth Bale ugani Santiago Bernabeu ni mambo ambayo yametishia kuvuruga uhusiano kati ya Florentino Perez ambaye ni Rais wa miamba hao na kocha Zinedine Zidane.

Bale, 30, alitarajiwa kuingia katika sajili rasmi ya Jiangsu Suning nchini China kwa mkataba wa miaka mitatu huku akipokezwa mshahara wa hadi kufikia kima cha Sh130 milioni kwa wiki.

Licha ya Zidane kushinikiza Kuondoka kwake, Perez alizuia uhamisho huo dakika za mwisho.

Huku presha ya kuongoza ufufuo wa kikosi hicho katika Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) na Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) ikizidi kumkosesha Zidane usingizi, dalili zote zinaashiria kwamba huenda mkufunzi huyo mzawa wa Ufaransa asidumu sana ugani Santiago Bernabeu.

Kulingana na magazeti mengi nchini Uhispania, hali hiyo inamweka kocha Jose Mourinho katika nafasi kubwa ya kurejea Bernabeu kudhibiti mikoba ya Real.

Hata hivyo, marejeo ya Mourinho huenda yakazima kabisa maazimio ya Pogba kuwahi kuvalia jezi za Real, kikosi ambacho amekuwa akikishabikia tangu utotoni.

Zidane hajaficha kabisa ukubwa wa kiu yake ya kujitwalia huduma za Pogba msimu huu. Ingawa hivyo, msukumo wake kwa usimamizi kuwashawishi Man-United zaidi kumwachilia kiungo huyo wa zamani wa Juventus kwa ofa nono zaidi huenda ukamtia pabaya kambini mwa waajiri wake.

Hamu kuchezea Real Madrid

Mnamo Juni 2019, Pogba alikiri kwamba kikubwa zaidi katika maazimio yake kitaaluma ni kuingia kambini mwa Real chini ya ukufunzi wa Zidane.

Hata hivyo, kima cha Sh21 bilioni zinazodaiwa na Man-United kwa minajili ya nyota huyo ni fedha ambazo Perez amesisitiza kwamba hawezi kumudu.

Miongoni mwa mambo yanayomsukuma Pogba kutaka kuingia katika sajili rasmi ya Real ni haja ya kuungana upya na familia yake. Nduguze wawili – Mathias na Florentin kwa sasa wanasakata soka ya kulipwa kambini mwa Manchego jijini Madrid.

Badala ya Pogba, matamanio ya Perez ambaye tayari amewasaidia Real kuwasajili Luka Jovic na Eden Hazard, ni kukiona kikosi hicho kikijinasia huduma za Christian Eriksen na Harry Kane wa Tottenham Hotspur pamoja na chipukizi Kylian Mbappe kutoka PSG.