Michezo

Mourinho na 'mwanawe' nguvu sawa katika EPL

November 30th, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

TOTTENHAM Hotspur walirejea kileleni mwa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Novemba 29 baada ya kuwalazimishia Chelsea sare tasa uwanjani Stamford Bridge.

Kipa Edouard Mendy wa Chelsea alifanya kazi ya ziada na kupangua makombora mazito aliyoelekezewa na Serge Aurier na Steven Bergwijn walioshirikiana vizuri na washambuliaji Harry Kane na Son Heung-min wa Tottenham.

Chelsea walishuka dimbani wakitawaliwa na kiu ya kusajili ushindi katika mchuano huo ulikokuwa wao wa 1,000 kusakata tangu umiliki wao utwaliwe na bwanyenye Roman Abramovich.

Baada ya uongozi wa EPL kuchukuliwa na Liverpool mnamo Novemba 28 kutokana na sare ya 1-1 dhidi ya Brighton, Tottenham walihitaji sare ili kutua juu ya mabingwa watetezi kwa wingi wa mabao. Sawa na Liverpool, Tottenham kwa sasa wanajivunia alama 21.

Ni pengo la alama mbili ndilo linatamalaki sasa kati ya nambari tatu Chelsea na viongozi wa jedwali la EPL.

Licha ya Chelsea kuwa miongoni mwa vikosi vinavyojivunia huduma za washambuliaji mahiri zaidi kwa sasa katika EPL – Hakim Ziyech, Timo Werner na Kai Havertz – masogora hao wa kocha Frank Lampard walishindwa kuvuruga ulinzi wa Tottenham uliojumuisha chipukizi Joe Rodon aliyekuwa akiwajibishwa na Mourinho kwa mara ya kwanza katika kikosi chake.

Huo ulikuwa mchuano wa nne mfululizo kwa Tottenham kukamilisha bila ya kufungwa bao. Kwa upande wao, Chelsea kwa sasa hawajapoteza mchuano wowote wa EPL tangu Septemba 20, 2020.

Chelsea tayari wanajivunia kufuzu kwa hatua ya 16-bora ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) zikisalia mechi mbili zaidi kwenye hatua ya makundi. Ufanisi huo unatarajiwa kuwapa motisha ya kutoa ushindani mkali zaidi kileleni mwa jedwali la EPL baada ya uwezo wao kudhihirika walipokomesha rekodi ya Tottenham ambao hadi Novemba 29, walikuwa wametandaza mechi tano kwa mpigo bila ya kupoteza hata moja.

Ushindi kwa Tottenham dhidi ya Chelsea ungaliwafanya kuwa miongoni mwa vikosi vya kupigiwa upatu wa kutwaa taji la EPL muhula huu ikizingatiwa kwamba walishuka ugani Stamford Bridge wakitawaliwa na ari kupepeta Manchester City 2-0 katika gozi la awali.