Michezo

Mourinho sasa halali akitamani Bale arejee uwanjani

September 27th, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

KOCHA Jose Mourinho amekiri kwamba hana uhakika kuhusu wakati ambapo sajili mpya Gareth Bale atarejea uwanjani kusakata soka, lakini amesema anatamani mno kumpa nafasi nyota huyo nafasi ya kudhihirisha ukubwa wa uwezo wake.

Raia huyo wa Wales alijiunga upya na Spurs kwa mkopo wa msimu mmoja kutoka Real Madrid mnamo Septemba 19, 2020.

“Sijui ni lini atarejea katika kiwango chake bora cha uchezaji. Lakini mara tu atakapopata nafuu, nitampa nafasi katika kikosi cha kwanza,” akatanguliza Mourinho.

“Ninachoelewa ni kwamba anatamani sana kucheza haraka iwezekanavyo. Amefurahia kurejea hapa baada ya kuifanyia klabu hii mambo makubwa kabla ya kuyoyomea Uhispania,” akasema kwa kusisitiza kwamba kwa kawaida, mchezaji anapokuwa na hamu ya kurejea uwanjani haraka, hupona pia upesi.

Nyota huyo raia wa Wales aliagana na Spurs mnamo 2013 baada ya kusajiliwa na Real kwa kima cha Sh11 bilioni. Akiwa Real, alifunga zaidi ya mabao 100 na kusaidia kikosi hicho kutwaa mataji manne ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

“Najihisi vizuri kurejea. Spurs ni klabu spesheli sana kwangu. Ndipo nilipojijengea jina kitaaluma,” akatanguliza.

“Natarajia kujinyanyua haraka iwezekanavyo na kusaidia Spurs kurejea wanakostahili kuwa na kuwanyanyulia mataji ya haiba chini ya Mourinho,” akaongeza.

Kwa mujibu wa Spurs, Bale alijiunga nao akiwa na jeraha la goti alilolipata wakati akichezea Wales mwanzoni mwa Septemba 2020.

“Tutaanza kumchezesha baada ya likizo fupi ya Oktoba itakayopisha mechi za kimataifa. Tunatarajia kwamba atakuwa amepona jeraha kufikia wakati huo,” ikasema sehemu ya taarifa ya Spurs.

Ina maana kwamba Bale atakosa jumla ya mechi tano zijazo za Spurs na gozi la kwanza atakalolisakata ndani ya jezi za waajiri wake ni dhidi ya West Ham mnamo Oktoba 17, 2020.

Kwa mujibu wa ripoti ya daktari wa Spurs, Bale atakosa michuano ya Spurs dhidi ya Shkendija katika pambano la Europa League, Newcastle United na baadaye Manchester United.

Iwapo ubashiri wa klabu utatimia, basi Bale huenda akarejea kutambisha waajiri wake dhidi ya West Ham United mnamo Octoba 17, mechi ambayo itafuatwa na nyingine dhidi ya Burnley halafu Brighton & Hove Albion.

Bale alisajiliwa na Spurs kwa mara ya kwanza mnamo 2007 kwa kima cha Sh700 milioni. Mbali na kunyanyua mataji manne ya UEFA akiwa Real, pia alisaidia miamba hao wa soka ya Uhispania kutwaa makombe mawili ya La Liga, moja la Copa del Rey, matatu ya Uefa Super Cup na mataji matatu ya Kombe la Dunia.

Bale anasalia kuwa mchezaji ghali zaidi katika historia ya soka ya Uingereza na ndiye Mwingereza (Wales) anayejivunia kufunga idadi kubwa zaidi ya mabao katika soka ya Uhispania. Anajivunia kuwafungia Real jumla ya mabao 80 na kuchangia mengine 40 katika jumla ya mechi 171 zilizopita.

Kiini cha kubanduka kwake Real ni kudorora kwa uhusiano kati yake na kocha raia wa Ufaransa, Zinedine Zidane.

Kwa kumsajili Bale kwa Sh11 bilioni, Real walivunja rekodi ya Sh10.8 bilioni walizoweka mezani mnamo 2009 kwa minajili ya huduma za nyota raia wa Ureno, Cristiano Ronaldo mnamo 2009.

Katika mkataba wake wa kwanza wa miaka sita, Bale alikuwa akilipwa na Real mshahara wa Sh42 milioni kwa wiki kabla ya kutia saini mkataba mwingine wa miaka sita mnamo 2016 ambapo alikuwa akilipwa Sh84 milioni kwa wiki.