Michezo

Moyes pua na mdomo kuiongoza West Ham United kukwepa shoka EPL

July 18th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

NAHODHA Mark Noble amesema West Ham United “wanastahili kusalia katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL)” na ushindi wa 3-1 waliousajili dhidi ya Watford mnamo Julai 17, 2020, ni ithibati tosha ya kiu yao katika kufanikisha azma hiyo.

Matokeo ya West Ham katika mchuano huo yaliwawezesha vijana hao wa kocha David Moyes kuchupa hadi nafasi ya 15 kwa alama 37 sawa na Brighton huku zikiwa zimesalia mechi mbili pekee ligini msimu huu.

Mchuano dhidi ya Watford ulikuwa wa 500 kwa Noble kuchezea West Ham waliompokeza malezi ya awali kabisa katika ulingo wa soka. Watford kwa sasa wapo katika hatari ya kushuka ngazi kwa pamoja na Bournemouth na Aston Villa baada ya Norwich City tayari kushushwa ngazi.

Kikubwa zaidi kinachowaning’iniza Watford padogo ni kwamba wamesalia na kibarua kigumu zaidi katika mechi za mwisho wa msimu huu dhidi ya Manchester City na Arsenal.

“Miaka 17 au 18 iliyopita, niliwahi kushikwa nikijaribu kuingia katika uwanja wa Upton Park kutazama mechi ya West Ham bila tiketi. Nilishtakia hali yangu na nikatwaliwa na akademia ya kikosi hicho ambacho kwa sasa nimekichezea mechi 500. Haya kwangu si mafanikio madogo. Kubwa zaidi ni kwamba kikosi hiki kinastahili kusalia katika kivumbi cha EPL,” akasema Noble.

Wakicheza dhidi ya Watford, West Ham walijipata kifua mbele chini ya dakika 10 za kipindi cha kwanza kupitia mabao ya Michail Antonio na Tomas Soucek aliyeshirikiana vilivyo na Jarrod Bowen.

Declan Rice alifanya mambo kuwa 3-0 mwishoni mwa kipindi cha pili kabla ya Troy Deeney kuwafutia Watford machozi kunako dakika ya 49.

Moyes ambaye ni mkufunzi wa zamani wa Man-United na Everton, aliteuliwa kuwa kocha wa West Ham kwa mara ya pili mnamo Disemba 2019 kikosi hicho kikijivunia alama moja pekee juu ya mduara wa vikosi kwenye hatari ya kushushwa ngazi.

Kuwadumisha West Ham katika kivumbi cha EPL msimu ujao kutakuwa ufanisi mkubwa kwa Moyes iwapo atawaongoza vijana wake kuwachabanga Man-United na Aston Villa katika mechi mbili za mwisho.