Michezo

Moyes sasa kufanya kazi ya ukocha akiwa nyumbani

September 25th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

LICHA ya David Moyes kuugua Covid-19, kocha huyo raia wa Scotland atasimamia mechi itakayowakutanisha West Ham United na Wolves katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Septemba 27, 2020 uwanjani London Stadium akiwa nyumbani kwake.

Haya ni kwa mujibu wa kocha msaidizi wa West Ham, Alan Irvine ambaye amethibitisha kuwa Moyes kwa sasa amejitenga nyumbani katika juhudi za kudhibiti msambao wa virusi vya corona.

Baada ya kupatikana na corona, Moyes kwa pamoja na wanasoka Issa Diop na Josh Cullen walilazimika kuondoka uwanjani London Stadium haraka iwezekanavyo kabla ya mechi iliyowakutanisha na Hull City kwenye Carabao Cup kupigwa mnamo Septemba 22, 2020.

Licha ya Moyes kufichua mpango wake wa kufanyia kazi nyumbani kwa siku kadhaa zijazo, Irvine ndiye atakuwa kwenye eneo la kocha kwa upande wa West Ham katika mechi zijazo.

“Kila kitu tutakachofanya uwanjani kuanzia sasa kitaidhinishwa na Moyes. Sisi uwanjani London Stadium tutasalia tu kutekeleza maagizo atakayokuwa akitoa akiwa nyumbani kwake,” akatanguliza Irvine.

“Hata hii taarifa rasmi tunayoitoa sasa kwa vyombo vya habari imeandaliwa na Moyes akiwa nyumbani. Atasalia kufanyia kazi nyumbani hadi atakapopona. Mimi na wenzangu kwenye benchi ya kifundi ni wajumbe tu,” akaongeza.

Kwa mujibu wa Irvine, Moyes na wachezaji Diop na Cullen hawakuonyesha dalili zozote za corona kabla ya kufanyiwa vipimo vya afya na kupatikana na ugonjwa wa Covid-19.