Dondoo

Mpangaji ahepa na mke wa 'caretaker'

July 13th, 2020 1 min read

Na TOBBIE WEKESA

KAWANGWARE, Nairobi

WAPANGAJI wa ploti moja mtaani humu walibaki vinywa wazi baada ya polo kuhepa na mke wa ‘caretaker’.

Inasemekana polo huyo alikuwa amekodi chumba kimoja katika ploti ambayo mume wa mwanadada alikuwa akisimamia.

Kulingana na mdokezi, kwa muda mrefu, polo alikuwa na uhusiano wa kipenzi na kipusa. Uhusiano ambao ulikuwa ukiendeshwa kwa siri mno japo baadhi ya wapangaji wakishuku na kumdokezea jamaa.

Duru zinasema tukio hili lilipofanyika, ‘caretaker’ alikuwa ameenda kudai kodi kutoka kwa wapangaji waliokuwa wakiishi katika jumba jingine la mwajiri wake.

Inadaiwa aliporejea, aliipata nyumba yake ikiwa wazi.

“Hii nyumba leo imenyamaza hivi kwani watu walienda wapi?” caretaker alishangaa.

Jamaa alipigwa na butwaa alipobaini kwamba, nguo za mkewe hazikuwepo. “ Umemuona mke wangu?” polo alimuuliza jirani yake.

Jirani alimuangalia kwa mshangao.

“Mimi nilifikiri mlikuwa pamoja! Vile uliondoka, mkeo alikufuata nyuma akiwa na polo anayeishi nyumba ile,” jirani alimueleza.

‘Caretaker’ alimueleza kwamba yeye alikuwa kwa shughuli zake tofauti.

“Basi mpigie simu yule jamaa aliyekuwa naye muulize,” jirani alimueleza.

Simu ya mke wake ilikuwa imezimwa. Polo pia hakuichukua simu yake alipopigiwa. Chumba cha polo vilevile kilikuwa wazi bila chochote ndani.

‘Caretaker’ alianza kutokwa na kijasho jembamba. Wapangaji kwenye ploti walianza kupata habari kuhusu kilichompata msimamizi wa ploti yao.

“Mkeo nilimuona na begi kubwa akienda. Jamaa anayeishi kwenye chumba kile alikuwa amembebea begi yake ndogo ya mkononi,” mpangaji mmoja alisikika akisema.

“Wewe tulikupasha habari kuhusu uhusiano wa mkeo na huyo jamaa ukapinga. Mkeo ameenda,” sauti nyingine ya mpangaji ilisikika.

‘Caretaker’ alishindwa aanzie wapi.

“Tafuta mke mwingine uoe. Huyo ameenda,” alielezwa.