Habari za Kitaifa

Mpango kuboresha kilimo cha mboga za kienyeji

April 7th, 2024 1 min read

KNA Na CHARLES WASONGA

SHIRIKA la Utafiti wa Kilimo na Ufugaji (Kalro) kwa ushirikiano na wadauhusika katika sekta ya kilimo, limeanzisha mradi unaolenga kuendeleza kilimo cha mboga za kienyeji za Kiafrika (AIV) Magharibi mwa Kenya.

Kalro inashirikiana na Chuo Kikuu cha Nairobi na kile cha North Carolina State (UCSU) kuanzisha mradi huu, kupitia ufadhili kutoka kwa Shirika la Amerika kuhusu Maendeleo ya Kimataifa (USAID) kutekeleza mradi huo katika kaunti za Kakamega na Kisii, japo kwa majaribio.

Kulingana na Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo Eliud Kireger, mradi huo unalenga kusuluhuhisha changamoto zinazokabili wakulima wadogo katika ukuzaji na uuzaji mboga hizo.

Kuna mseto wa mboga za kienyeji, kuanzia mnavu maarufu kama sucha au managu, mchicha – terere, kunde, murenda na saga, miongoni mwa zingine.

Mkulima akielezea kuhusu ukuzaji mboga za kienyeji aina ya managu. PICHA|SAMMY WAWERU

“Wale tunaolenga zaidi chini ya mradi huu ni wanawake na vijana ili wawezae kukuza na kuuza AIV nchini Kenya,” Dkt Kireger akasema mnamo Ijumaa, Aprili 5, 2024 akiwa Kaunti ya Kakamega wakati wa uzinduzi wa mradi huo.

Alieleza kuwa kando na mboga hizo kuwa na umuhimu wa kitamaduni, zina utajiri mkubwa wa madini bora na faafu kwa mwili.

Hata hivyo, afisa huyo alisema licha ya kwamba mboga hizo ni zenye thamani kubwa, zimebaguliwa, za kisasa zikiangaziwa zaidi.

Mboga za kienyeji zinaweza kukaushwa, uongezaji thamani, hatua ambayo ikikumbatiwa kikamilifu itasaidia kuangazia kero ya njaa msimu wa ukame na kiangazi.

Mboga zilizokaushwa. PICHA|SAMMY WAWERU