Mpango maalumu wa Rais kupanda miti kwa ajili ya uhifadhi wa mazingira

Mpango maalumu wa Rais kupanda miti kwa ajili ya uhifadhi wa mazingira

NA SAMMY WAWERU

AFISI ya Rais imezindua mpango maalum unaolenga kufanikisha upanzi wa miti nchini.

Mpango huo aidha unashirikisha asasi za serikali, sekta za kibinafsi na mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO).

Rais William Ruto ameweka shabaha ya upandaji miti bilioni 15, chini ya kipindi cha muda wa miaka 10 ijayo.

Awamu ya kwanza ya mpango huo, Special Presidential Forestry and Rangeland Acceleration Program, itatekelezwa kati ya 2022 – 2027.

Awamu ya pili, itakuwa kati ya 2027 na 2032.

“Kwa sasa uhifadhi wa miti umefika asilimia 12.13, na mpango maalumu wa Rais utasaidia kugonga asilimia 30 kufikia 2032,” Bw Julius Kamau, Mhifadhi Mkuu wa Misitu, Shirika la Huduma za Misitu Nchini (KFS) ameambia Taifa Leo.

Ni shabaha ambayo itafanikishwa endapo kila Mkenya atajitolea, Kamau akisema serikali kuu na zile za kaunti zitashirikiana kwa karibu.

“Nusu ya idadi hiyo itafadhiliwa na serikali, na inayosalia sekta za kibinafsi, NGO na wananchi,”afisa huyo akaelezea.

Bw Kamau alisema tayari KFS imepata zaidi ya washirika 100, kutoka sekta ya kibinafsi na mashirika yasiyo ya kiserikali.

Rais William Ruto amezindua mpango maalum kupanda miti nchini. PICHA | SAMMY WAWERU

Shirika hilo aidha linahimiza taasisi za serikali zenye mashamba makubwa, kutenga asilimia 30 ya ardhi kupandwa miti.

Ukataji miti na uharibifu misitu umetajwa kama mojawapo ya kiini kikuu cha mabadiliko ya tabianchi.

Janga la ukame ni mojawapo ya athari zinazotokana na tabianchi, mgeuko wa hali ya hewa.

Aidha, Upembe wa Afrika, Kenya ikiwemo umeathirika pakubwa.

  • Tags

You can share this post!

Bei ya omena kupanda wavuvi wakitii marufuku

Hafla ya kufuzu kwa mahafali 5,000 yafana chuoni MKU

T L