Habari Mseto

Mpango unaolenga kuwainua vijana kupanuliwa zaidi

June 11th, 2020 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

MPANGO wa Kazi kwa Vijana utaendelea katika kaunti zingine ili vijana waweze kujikimu kimaisha.

Waziri msaidizi wa Huduma za Umma, Vijana na Jinsia Rachel Shebesh alisema Jumatano kwamba kwa wakati huu mradi huo unaendelea katika kaunti nane hapa nchini.

Alisema wakati huu watu wanapokabiliana na janga la Covid-19 kumeshuhudiwa kudhulumiwa kwa wanawake, wasichana na hata wanaume nyumbani.

“Imebainika kuwa wakati huu wa kukabili Covid-19 watu wanapitia masaibu mengi kutokana na ukosefu wa pesa. Kwa hivyo vijana wengi watanufaika na mpango huu wa Kazi kwa Vijana,” alisema Bi Shebesh.

Alisema serikali ina mipango ya kuwapa mikopo wale walioathirika kupitia fedha za uwezo Fund na Enterprise Fund.

Alisema serikali inafanya mikakati kuona ya kwamba watu wanaodhulumiwa wanalindwa hasa wakati huu wa janga la Covid-19.

Kamishna wa kaunti ya Kiambu, Bw Wilson Wanyanga alisema awamu ya pili ya kuajiri vijana itazinduliwa na Rais Uhuru Kenyatta mnamo Julai mosi 2020.

Alisema mradi huo umenufaisha vijana wapatao 2,300 katika Kaunti ya Kiambu.

Alisema katika awamu ya pili, wanatarajia kuajiri vijana 23,881 katika Kaunti ya Kiambu na wasimamizi wao 1,092.

“Wakati wa uzinduzi wa awamu ya pili, vijana wapatao 200,000 wanatarajiwa kuajiriwa kote nchini,” alisema Bw Wanyanga.

Alisema baadhi ya kaunti zinazoendesha mradi huo kwa sasa ni Nairobi, Kiambu, Kisumu, Nakuru, Mandera, na Kwale.

Aliwapa matumaini vijana kwa kuwahakikishia kuwa wakati huu wataajiri wale hawakupata nafasi wakati wa awamu ya kwanza.

Alisema kazi maalum wanazostahili kuendeleza ni kufyeka nyasi mitaani, upakaji wa rangi katika kuta za majumba, kujenga vyoo mitaani, na pia kuzibua mfumo wa majitaka.

Alisema vijana hao pia watafunzwa maswala kama vile kutoa huduma ya kwanza na mambo mengine muhimu.

Bw Mugo Kimani ambaye ni miongoni mwa vijana walioajiriwa alisema amenufaika pakubwa kutokana na ajira hiyo chini ya mpango wa Kazi kwa Vijana.

“Kwa wakati huu ninaweza kujikimu kimaisha kwa kulea watoto wawili na kumtunza mke wangu. Tunaiomba serikali izidi kutuongeza muda wa kufanya kazi hiyo,” alisema Bw Kimani.