Habari MsetoSiasa

Mpango wa ANC, Ford-K kuungana wasambaratika

November 1st, 2018 2 min read

Na SHABAN MAKOKHA

TANGAZO la naibu kiongozi wa Ford-Kenya, Boni Khalwale kwamba, atamuunga mkono Naibu Rais William Ruto kuwania urais mnamo 2022 limetishia mchakato wa kuunganisha chama hicho na kile cha Amani National Congress (ANC).

Vyama hivyo, ambavyo vinaongozwa na Seneta Moses Wetang’ula (Bungoma) na Bw Musalia Mudavadi mtawalia vilikuwa vimetangaza kwamba vinapanga kuungana ili kubuni chama kipya, All Kenyan Alliance (AKA).

Wikendi iliyopita, Dkt Khalwale alitangaza kwamba, mpango huo ulikuwa ukingoja kupitishwa na viongozi hao wawili ili kutekekezwa rasmi.

Hata hivyo, Katibu Mkuu wa ANC, Barack Muluka alisema kuwa kuingizwa kwa Bw Ruto katika mpango huo huenda kukausambaratisha.

Bw Muluka na Dkt Khalwale ndiyo wanaongoza kundi maalumu linalohusika katika mchakato wa kuunganisha vyama hivyo viwili.

“Sifahamu lolote kuhusu tangazo la Dkt Khalwale. Sielewi alivyomaanisha hata kidogo,” akasema Bw Muluka.

Wiki iliyopita, Khalwale alitangaza wazi kwamba Bw Ruto ndiye mgombea mkuu wa urais, huku akiahidi kumpigia kura.

Na Jumamosi iliyopita, kiongozi huyo alirejelea kauli iyo hiyo, akiashiria kwamba mchakato huo umekamilika na kwamba, chama hicho kipya kitatumika na jamii ya Waluhya kumsimamisha mgombea urais katika uchaguzi huo.

Taharuki ya ni nani atakayeteuliwa kukiongoza chama hicho na yule atakayekuwa mgombea urais wa jamii ya Abaluhya ni sababu pia zinazotajwa kuathiri kutangazwa kwa chama hicho kipya.

Mbunge Maalumu Godfrey Osotsi anashikilia kuwa mchakato huo umejawa na hali ya kutoaminiana na ukosefu wa mkakati thabiti kuhusu malengo yake.

“Chama cha ANC kinakumbwa na mzozo wa uongozi, ambao uko mahakamani kwa sasa. Nafasi anayoshikilia Bw Muluka si halali, hivyo hana mamlaka yoyote kutia saini mkataba wa muungano kati ya vyama hivyo viwili,” akasema Bw Osotsi.

Mbali na hayo, alisema mchakato huo unakumbwa na tofauti kubwa za kisiasa, kwani ANC inaonekana kutiwa wasiwasi na msimamo wa Ford-Kenya kuunga mkono azima ya Bw Ruto kuwania urais mnamo 2022.

Mbunge huyo alisema licha ya kuonyesha umoja wao hadharani, Mabw Mudavadi na Wetang’ula wana tofauti kubwa za kisiana kati yao. Bw Osotsi amekuwa akizonania nafasi ya ukatibu mkuu wa ANC na Bw Muluka.

Hata hivyo, Dkt Khalwale alitaja chama hicho kama “nguvu mpya ya kisiasa” katika eneo la Magharibi.

“All Kenyan Party ndicho chama kipya kufuatia kuungana kwa Ford Kenya na ANC. Tunawaomba Wakenya wote kujiunga nacho ili kuleta mageuzi ya uongozi nchini,” akasema.

Alisema hayo Jumanne kwenye mazishi ya Bw Jacob Nanjakululu, kijiji cha Makhima, Kaunti ya Kakamega.