Mpango wa ‘Happy Hour’ warejeshwa kupunguza msongamano Mombasa

Mpango wa ‘Happy Hour’ warejeshwa kupunguza msongamano Mombasa

Na Mohamed Ahmed

SERIKALI ya kaunti ya Mombasa imerudisha mpango wa kupunguza msongamano wa magari kupitia mtindo unaojulikana kama ‘Happy Hour’.

Mtindo huo unahusishwa kufungwa kwa sehemu moja ya barabara na kuruhusu magari kutumia upande mwengine kwa dakika za kuhesabu.

Mpangilio huo umekuwa maarufu upande wa kutoka Mombasa Kisiwani kuelekea maeneo ya Nyali na Kisauni.Wakati virusi vya corona vilipozuka, mtindo huo ulikuwa umesimamishwa.

Hata hivyo kwa wiki moja sasa mpango huo umeonekana kurudi tena.Hii ni baada ya waziri wa masuala ya uchukuzi na miundo msingi Geoffrey Nato kupitia notisi ya gazeti la serikali kuwa barabara zitaanza kufungwa tena ili kuruhusu mpango huo kuendelea.

Katika notisi hiyo, Bw Nato alielekeza kuwa barabara ya kutoka Mombasa Kisiwani itafungwa kwa muda usiozidi dakika 15 kuruhusu magari kupita.

Mpango utafanyika muda wa saa kumi na moja jioni hadi saa kumi na mbili na nusu jioni kila siku ya wiki na saa moja na nusu asubuhi hadi saa tatu asubuhi.

Barabara hizo ni pamoja na ile ya Sheikh Abdullah Farsi mpaka kwenye daraja la Nyali na kuelekea barabara ya Fidel Odinga.Barabara inayoshikana na mzunguko wa Mamba pia itafungwa.

Barabara nyengine ambazo zitaathirika na mpango huo ni pamoja na New Malindi Road, Ronald Ngala Road, Tom Mboya Junction na barabara ya Narok.

You can share this post!

Mutua alia Kalonzo ameteka BBI Ukambani

Kila familia kulipa Sh6,000 katika mageuzi mapya NHIF