Habari

Mpango wa Kazi Mtaani wazinduliwa rasmi Garissa vijana 4,481 wakipata nafasi hizo

July 14th, 2020 1 min read

Na FARHIYA HUSSEIN

KAUNTI ya Garissa imejiunga na baadhi ya kaunti nyinginezo nchini ambako kumezinduliwa rasmi mpango wa Kazi Mtaani.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo katika uwanja wa michezo wa Shule ya Msingi ya Garissa, Katibu wa Kaunti ya Garissa, Bw Abdi Ali alisema jumla ya vijana 4,481 walichukuliwa kutoka kaunti hiyo.

“Vijana hao wataajiriwa na kufaidika kutokana na mpango huo ambao utatekelezwa na idara inayosimamia mipango wa miji na Huduma ya Vijana ya Kitaifa,” alisema Bw Ali.

Programu hiyo ilianzishwa na Rais Uhuru Kenyatta kama njia ya kuwapa vijana nafasi za kujikimu kimaisha.

Bw Ali alisema mpango huo utahusisha usafishaji wa vichaka vya mathenge ambavyo vimekuwa kero na hatari katika mji wa Garissa.

“Mpango huu utawasaidia vijana kujikimu kujinasua kutoka hali ngumu ya kiuchumi kipindi hiki cha janga la corona ambalo liliathiri vibaya maisha ya watu,” alisema.

Wakati huo huo, alikuwa pamoja na Mkuu wa Eneo la Kaskazini Mashariki, Bw Nicodemus Ndalana ambaye aliwasihi vijana kutumia mapato watakayopata kwa njia ya Mpesa kwa busara.

Bw Ndalana aliongezea kuwa lengo kuu la mpango huo ni kuwawezesha vijana kujikimu na kuhakikisha uwepo wa mazingira safi katika kaunti hiyo.

“Baadhi ya kazi watakazofanya ni uzoaji taka, usafishaji wa barabara na maeneo ya umma, kuzibua mifereji ya majitaka na kusafisha njia,” alisema Bw Ndalana.