Habari Mseto

Mpango wa KFS kuzindua huduma za feri Ziwa Turkana

March 21st, 2019 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

KUNA mpango wa serikali kuanzisha huduma za uchukuzi kwa njia ya feri katika Ziwa Turkana.

Hii ni baada ya Bodi ya Wakurugenzi wa Huduma za Feri Kenya (KFS) kuidhinisha kuanzishwa kwa huduma hizo katika kaunti zingine zaidi ya Mombasa.

KFS imepanga kupanua huduma zake hadi Diani (Kwale), Malindi (Kilifi) na Lamu katika eneo la Pwani na Ziwa Victoria na Ziwa Turkana.

Meneja Mkurugenzi wa KFS Bakari Gowa alisema mapendekezo ya kupanuliwa kwa huduma hizo yamewasilishwa kwa Wizara ya Uchukuzi.

“Mapendekezo hayo yalithibitishwa kwa kiwango chetu na bodi ya wakurugenzi na sasa tunangoja kuidhinishwa na Wizara kabla ya kuendelea na mipango zaidi,” alisema Bw Gowa.

Bw Gowa alisema upanuzi wa huduma hizo utatekelezwa kwa awamu mbili, ambapo awamu ya kwanza itahusu operesheni lamu na Diani kabla ya kuanza mpango huo Turkana na Kisumu katika awamu ya pili ambayo inahusu huduma katika Ziwa Victoria na Ziwa Turkana.

“Maafisa wetu walifanya majadiliano na Kaunti za Homabay na Kisumu ambazo zimeonyesha kupendezwa na mpango huo. Kaunti ya Homabay tayari imejitolea kwa mpango huo,” alisema Bw Gowa.

Mpango huo utatekelezwa kupitia kwa ushirika kati ya mashirika ya kibinafsi, serikali na umma (PPP) ikiwa utaidhinishwa. Bw Gowa alisema wanatafuta washirika katika kutekeleza mpango huo.