Habari

Mpango wa kuanzisha mitihani ya kitaifa kwa wanafunzi wa gredi ya tatu ungalipo – Magoha

August 23rd, 2019 2 min read

Na GAITANO PESSA na SAMMY WAWERU

WAZIRI wa Elimu Profesa George Magoha amesema Ijumaa kuwa serikali kuu inafanya kila iwezalo kuhakikisha kuwa mpango wa kuanzisha mitihani ya kitaifa kwa wanafunzi wa gredi ya tatu unazinduliwa Januari 2020.

Amesema hayo mnamo wakati ambapo gumzo kote nchini kwa sasa ni kuhusu shughuli ya kuhesabu idadi ya Wakenya itakayofanyika Jumamosi.

Akiongea katika Shule ya Msingi ya Moody Awori eneobunge la Funyula, Kaunti ya Busia wakati wa kukagua jinsi ambavyo mafunzo ya mfumo mpya wa elimu unaojikita katika umilisi (CBC) kwa walimu, waziri amesema kuwa wameweka mikakati ya kutosha kuhakikisha kuwa walimu wanahitimu waweze kufunza kwenye mfumo huo.

Aidha, Waziri Magoha amesema kuwa serikali kuu imejizatiti kuimarisha miundomsingi katika shule za upili ikizingatiwa kuwa wanafunzi watachukua muda wa miaka sita kulingana na mfumo huo.

“Ninawarai washikadau husika kushirikiana na serikali kuu kupitia kwa Wizara ya Elimu ili kufanikisha CBC,” amesema waziri Magoha.

Kuhusu sensa; shughuli ya kuhesabu Wakenya itakayofanyika kuanzia kesho Jumamosi na kuendelea usiku kucha, waziri amewahimiza raia kushiriki kikamilifu ili kurahisisha mipango ya serikali.

Amesisitiza kuwa shule zote zitasalia kufungwa hadi shughuli hiyo kukamilika.

Wakati uo huo waziri huyo ametoa ufadhili wa Sh10 milioni kutoka kwa Rais Uhuru Kenyatta ili kusaidia katika ujenzi wa shule ya msingi ya Moody Awori.

Matayarisho ya sensa

Taifa likijiandaa kushiriki shughuli ya kuhesabu watu, sensa 2019, maafisa wa muda wa Shirika la Takwimu Nchini (KNBS) Ijumaa wameendelea na matayarisho katika kipindi cha lala salama.

Kulingana na KNBS litafanyika kati ya saa kumi na mbili za jioni hadi kumi na mbili asubuhi.

Baadhi ya mitaa tuliyozuru kaunti ya Nairobi na Kiambu, maafisa wa muda wa KNBS walikuwa katika harakati za kutamatisha maandalizi na kujaribu utendakazi wa mashine zitakazotumika kunakili data.

“Tuko katika awamu ya mwisho kufanyia mashine jaribio pamoja na kutambua majumba,” afisa mmoja eneo la Zimmerman, Nairobi, na aliyeomba kubana jina lake kwa sababu haruhusiwi kuzungumza na vyombo vya habari ameambia Taifa Leo.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia Joe Mucheru Alhamisi alisema data za sensa zinalenga kujua jumla idadi ya Wakenya, ambapo itasaidia serikali katika ugavi wa raslimali, kufanya maendeleo katika kiwango cha kitaifa na serikali za ugatuzi.

Bw Mucheru maelezo ya sensa ni ya kina yakilinganishwa na ya Huduma Namba, shughuli iliyofanywa kati ya Aprili na Mei 2019.

Afisa aliyezungumza na Taifa Leo kuhusu maandalizi yake aliuliza mmoja wa mpangaji Zimmerman “majina na kiongozi wa boma-familia”.

Aidha, alinakili maelezo hayo kwenye kipakatalishi, na kutia maandishi kwenye mlango.

Alhamisi jioni maafisa kutoka kituo cha polisi cha Zimmerman walizuru majengo ya upangaji wakitia vibango vya sensa mwaka 2019 kwenye milango na malango.

Shughuli sawia na hiyo imeshuhudiwa mtaa wa Mumbi, Mwihoko, Progressive na Maguo, Kaunti ya Kiambu.

Maafisa watakaoendesha shughuli hiyo watakuwa na sare maalum, hasa koti linalomeremeta na lenye nembo ya KNBS, ambapo wataandamana na maafisa wa polisi, machifu na wazee wa mitaa. Pia, watakuwa na kitambulisho kutoka shirika hilo la takwimu.

Kwa mujibu wa sensa ya 2009, Kenya ilikuwa na jumla ya wananchi milioni 38.6. Mwaka huu inapaniwa huenda idadi ikawa zaidi ya milioni 45.