Mpango wa Raila, Ruto kuungana wapata pingamizi

Mpango wa Raila, Ruto kuungana wapata pingamizi

Na SHABAN MAKOKHA

BAADHI ya wabunge kutoka eneo la Magharibi wamepuuza uwezekano wa Naibu Rais William Ruto kuungana na kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga wakisema viongozi hao wawili wamekuwa mahasimu wakubwa wa kisiasa.

Walisema kwamba wawili hao wamekuwa wakishambuliana vikali hatua ambayo imesababisha watu kufutwa kazi serikalini.

Mbunge wa Mumias Mashariki, Bw Benjamin Washiali na mwenzake wa Likuyani, Dkt Enoch Kibunguchy walidai kwamba Bw Odinga anapenda siasa za kuvuruga watu ambazo kulingana nao zilifanya wandani wa Dkt Ruto kupokonywa nyadhifa za uongozi bungeni na kamati za bunge.

Kulingana na Bw Washiali, iwapo naibu rais atakubali kuungana na Bw Odinga, basi anafaa kujiandaa kwa usaliti ambao utakuwa mwisho wa azma yake ya kisiasa kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Dkt Ruto ametangaza kuwa atagombea urais kwenye uchaguzi mkuu wa 2022 na anatumia kila mbinu kutimiza azma yake.

Tayari, amewarai viongozi wa kidini, wanawake na vijana, na amekuwa akitoa pesa akitembelea maeneo yaliyo na idadi kubwa ya kura tangu 2013 kupitia vuguvugu lake la ‘hasla’.

“Hata kama katika siasa lolote linawezekana, haitafurahisha baadhi yetu ambao tuliteseka tangu Bw Odinga alipokutana na Rais Uhuru Kenyatta wakasalimiana kuona kiongozi wetu, William Ruto, akiungana na Tinga. Hakutakuwa na uaminifu katika muungano kama huo,” alisema Bw Washiali.

Mbunge huyo alikuwa kiranja wa wengi katika bunge la kitaifa tangu 2017 hadi Juni mwaka jana alipopokonywa wadhifa huo pamoja na wandani wengine wa Dkt Ruto.

Alisema kwamba nyota ya kisiasa ya Dkt Ruto inaendelea kung’aa na hafai kuhusika na Bw Odinga kabla ya uchaguzi mkuu ujao.

Washirika wa kiongozi wa chama cha Ford Kenya, Moses Wetang’ula na wa ANC, Musalia Mudavadi wanamhimiza Dkt Ruto kujiunga na muungano wa One Kenya Alliance wa

Mudavadi, Wetang’ula, Kalonzo Musyoka na Gideon Moi badala ya kuungana na Bw Odinga.

Dkt Kibunguchy alimhurumia Dkt Ruto akisema ameumizwa kisiasa na siasa za Bw Odinga.

“Wakati Ruto alipojitolea kutetea ushindi wa Bw Odinga 2007, alijipata katika Mahakama ya Kimataifa kuhusu Uhalifu iliyo The Hague. Nini kingine anafikiria atapata akiungana na Bw Odinga?”

“Wakati Dkt Ruto alipelekwa The Hague, Bw Odinga hakuonyesha majuto hata na badala ya kusimama naye, alimwambia abebe msalaba wake mwenyewe,” alisema Dkt Kibunguchy.

Alisema kwamba kuna chuki kubwa kati ya viongozi hao wawili na wakishirikiana, hali itakuwa mbaya zaidi.

Alimuomba Dkt Ruto kufikiria tena hatua yake kabla ya kuamua kuweka mkataba wa kubuni muungano wa kisiasa na Bw Odinga. Badala yake alimshauri kushirikiana na viongozi wasiojipenda na waaminifu kupitia One Kenya Alliance.

“Badala ya kushirikiana na mtu ambaye tayari amewahi kukusaliti, naibu rais anafaa kuacha kiburi na kujiunga na One Kenya Alliance- ambao ni salama na bora kuliko muungano wake na Bw Odinga,” alisema Bw Kibunguchy akiongea na wanahabari katika kanisa la Vinyinya Church, Likuyani jana.

Alisema kwamba Bw Odinga aliwadanganya Mabw Kalonzo, Wetangula na Mudavadi kwenye chaguzi zilizopita kisha akawatema na kuanza kuwaita kupe.

You can share this post!

Upanuzi wa uwanja wa ndege wa Manda waanza

Wanabiashara wapigia debe chama cha Pwani