HabariSiasa

Mpango wa Ruto kumvua Matiang'i uwaziri waanikwa

May 20th, 2019 2 min read

Na MWANDISHI WETU

NAIBU wa Rais William Ruto na wafuasi wake wanatumia sakata ya dhahabu feki kujinufaisha kisiasa na kupanga kuondolewa afisini kwa waziri wa usalama wa ndani Dkt Fred Matiang’i.

Hii ni kulingana na kiongozi wa wachache bungeni John Mbadi, ambaye Jumatatu alisema kuwa tayari kuna wabunge wawili ambao wanaandaa mswada wa kutaka waziri huyo abanduliwe.

Akizungumza bungeni, Bw Mbadi alisema Dkt Ruto anapanga kutumia sakata hii kusukuma ajenda ya waziri Matiang’i aondolewe afisini, ili kulipiza kisasi cha Dkt Matiang’i kuteuliwa kuwasimamia mawaziri, nafasi ambayo ilionekana kumdunisha machoni pa Wakenya.

“Naibu wa Rais na timu yake wamekataa kuachia Mkurugenzi Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI) na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) fursa ya kufanya uchunguzi kuhusu suala hili na badala yake wanalitumia kupiga siasa na kumlenga Fred Matiang’i ili aondolewe afisini.

“Tunajua anayelengwa na Ruto na timu yake ni Matiang’i,” Bw Mbadi, ambaye pia ni mbunge wa Suba akasema.

Bw Mbadi aliendelea kusema: “Nina habari kuwa wabunge wawili; kutoka kusini mwa bonde la ufa na Murang’a wanaandaa mswada wa kutaka Matiang’i ang’olewe afisini.

“Suala la dhahabu feki linatumiwa tu kama kijisababu, lakini ukweli ni kuwa Ruto na timu yake hawajakuwa na furaha tangu wakati Matiang’i aliteuliwa kuwa akiwaongoza mawaziri na sasa wanaona suala hili kuwa muafaka kabisa kumtaka aondolewe afisini.”

Mbunge huyo alisema mpango wa mrengo huo hautafanikiwa, akisema wako tayari kuwakabili watakaouwasilisha, na kuongeza kuwa “Wakenya wamemkubali waziri Matiang’i kuwa waziri anayechapa kazi zaidi, hivyo waache kutafuta vijisababu vya kutaka aondolewe.”

Bw Mbadi alisema Naibu wa Rais na wafuasi wake hawana haja na Rais Uhuru Kenyatta ama kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga ambao pia wametajwa katika sakata hiyo, akisema lengo lao ni Dkt Matiang’i.

Mbunge huyo alisema hali ya Dkt Ruto kuchapa siasa sana imeanza kuathiri utendakazi wa serikali, akisema “Naibu wa Rais anafanya siasa sana hivi kwamba inakuwa vigumu kwa serikali kufanya kazi. Kulenga waziri kwa kuwa anadhani ni kizingiti kwake kufika ikulu si haki.”