HabariSiasa

Mpasuko kisiasa ulichangia Uhuru kufuta ziara ya Murang'a – Kang'ata

November 11th, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

SENETA wa Murang’a Irungu Kang’ata ameungama kwamba mgawanyiko miongoni mwa viongozi wa kisiasa katika kaunti hiyo ndio huenda ulisababisha Rais Uhuru Kenyatta kufutulia mbali ziara yake Jumapili.

Akiongea katika studio za runinga moja ya humu nchini Jumatatu asubuhi, Bw Kang’ata pia alizungumzia kuahirishwa kwa ziara ya Naibu Rais William Ruto katika kaunti hiyo siku hiyo hiyo ya Jumapili.

Bw Kang’ata alisema ziara ya viongozi hao wawili ilipangwa na makundi tofauti ya viongozi na hakuna kundi lililojulisha jingine.

“Makundi haya tofauti yalipanga mikutano hii, bila kushauriana kwa sababu yanatofautiana kisiasa. Viongozi waliopanga mkutano wa Rais ni wale wanaunga mkono muafaka kati yake na kiongozi wa ODM Raila Odinga na wale waliopanga ziara ya Dkt Ruto wanapinga muafaka huu huku wakipigia debe azma yake ya kuingia Ikulu 2022,” akasema Bw Kang’ata.

Rais Kenyatta aliahirisha ziara yake dakika za mwisho Jumapili na badala yake akawatuma mawaziri watatu; Fred Matiang’i (Usalama wa Ndani), Joe Mucheru (ICT) na James Macharia (Uchukuzi) kumwakilisha.

Alikuwa amepangiwa kuhudhuria ibada ya Jumapili katika Kanisa la Kianglikana (ACK) la Kenol, eneobunge la Maragua, na baadaye kuongoza harambee katika kanisa hilo.

Naye Dkt Ruto alikuwa amepangiwa kuhudhuria ibada ya Jumapili katika eneo bunge la Kandara kwa mwaliko wa mbunge wa eneo hilo Esther Wahome.

Lakini kulingana na Seneta Kang’ata, ziara ya Rais Kenyatta Murang’a Jumapili ilianza kupangwa mwezi Machi mwaka huu.

“Tulikuwa tumeenda Ikulu ya Nairobi kupokea basi la shule moja ndipo tukamwomba Rais atutembelee. Tulikuwa viongozi wengi kutoka Kaunti ya Murang’a,” akaeleza.

Bw Kang’ata alisema walipata thibitisho, kuhusu ziara ya Rais Kenyatta, mnamo Alhamisi.

“Lakini tulipata habari dakika za mwisho Jumapili kwamba rais hangeweza kufika,” akasema.

Hata hivyo, Bw Kang’ata alikana madai kuwa Rais Kenyatta anajitenga na watu wa Murang’a akisema serikali ya Jubilee imetekeleza miradi mingi zaidi yenye manufaa kwa wakazi.

“Miradi mingi ambayo serikali imetelekeleza katika kaunti yetu ya Murang’a ni thibitisho tosha kwamba Rais Kenyatta anawathamini zaidi,” akasema.