Akili Mali

Mpeketoni wapambana kuamsha kilimo cha pamba

May 2nd, 2024 3 min read

NA KALUME KAZUNGU

KILIMO cha pamba kilichonoga eneo la Mpeketoni katika Kaunti ya Lamu miaka ya sabini (1970s) kilififia na kusambaratika na hivyo kuwa zilipendwa, hasa kufikia mwaka wa 2000.

Ila juhudi zinazoendelezwa kwa sasa zinaashiria kuwepo kwa mwanga wa matumaini kwamba kilimo hicho kitainuka tena.

Miaka zaidi ya 50 iliyopita, Mpeketoni na eneo jirani la Witu, yote yakipatikana Lamu Magharibi, yalikuwa maeneo yaliyovuma kwa kuzalisha pamba ya hadhi nzuri nchini.

Ni maeneo hayo hayo ya Mpeketoni na Witu ambayo yaliwezesha Lamu kuzalisha na kusambaza pamba zaidi ya tani 5,000 kila mwaka.

Kati ya mwaka 1972, punde skimu ya Mpeketoni ilipoanzishwa hadi 1996, kilimo cha pamba kilinoga si haba kwani ndilo zao la kibiashara lililothaminiwa na wakulima wengi wa Lamu kuwaletea mtaji.

Licha ya wakulima wengi wa eneo hilo kuwa na hamu na mshawasha wa kuendelea kulikuza pamba, changamoto zilizokuwepo za ukosefu wa soko, bei duni na pia mbegu mbaya zilikabili kilimo hicho.

Kati ya mwaka 1998 na 2000, wakulima wa pamba, hasa Mpeketoni, walianza kuvunjika moyo kwani kilo ya pamba kwa wakati huo walikuwa wakiiuza kwa Sh14 pekee.

Hali hiyo ilishuhudia wakulima wengi wakisitisha kilimo hicho na kugeukia ukulima wa mimea mingine ya kuwapatia mtaji wa haraka, ikiwemo mahindi, korosho, maharagwe, zingifuri nakadhalika.

Ni mwaka huo wa 2000 ambapo kilimo cha pamba Mpeketoni, kilisambaratika kabisa.

Juhudi za wakulima wachache kujaribu kukifufua kilimo hicho kwa karibu miaka kumi iliyofuata aidha zilisalia kuwa ‘zilipendwa’ kwani mbali na changamoto ya soko, wadudu pia walianza kuifagilia pamba iliyokuwa ikikuzwa na wakulima hao wachache.

Usambazaji wa mbegu duni ya pamba miongoni mwa wakulima wa Mpeketoni pia ni kizingiti kingine kilichokabili sekta hiyo.

Katika mahojiano na Taifa Leo Alhamisi, Mwenyekiti wa Muungano wa Wakulima wa Pamba, Kaunti ya Lamu, Bw Joseph Mwangi Migwi, alisema mwanga wa matumaini kwamba kilimo cha pamba kingefufuka tena Mpeketoni ulianza kuonekana mwaka 2016.

Bw Migwi anamkumbuka Waziri wa Kilimo nchini kwa wakati huo, Bw Willy Bett, ambaye alitangaza azma ya Kenya kukifufua kilimo cha pamba.

“Twashukuru sana Waziri wa zamani wa kilimo, Willy Bett. Huyo ndiye aliyewatia moyo wakulima wa pamba Mpeketoni kuendelea kukuza zao hilo. Kilimo kilikuwa kimesambaratika. Twazitambua juhudi zake za 2017, ambapo aliagiza mbegu shwari ya pamba na yenye hadhi kutoka India, ambapo ilituwezesha sisi wakulima kuanza kupata mazao mazuri,” akasema Bw Migwi.

Kufikia sasa Lamu imepiga hatua kubwa katika kilimo cha pamba, ambapo ina zaidi ya wakulima 10,000 wapatikanao maeneo ya Mpeketoni, Baharini, Mkunumbi, Hongwe, Witu na Hindi-Magogoni.

Pia juhudi zinafanywa kuendeleza kilimo cha pamba kwenye maeneo ya visiwa, kaunti ya Lamu, ikiwemo Faza na Pate, Lamu Mashariki.

Bw Migwi anasema miongoni mwa vigezo vinavyowapa matumaini wakulima kuendelea kujitosa kwenye kilimo cha pamba ni kupanda kwa bei, ambapo kwa sasa kilo moja ya zao hilo imekuwa ikiuzwa kwa kati ya Sh30 na Sh37.

Hatua nyingine iletayo mwanga wa matumaini kwa wakulima ni kuwepo kwa soko tayari.

Hii inatokana na wadau mbalimbali wa sekta ya pamba, ikiwemo kiwanda cha pamba cha Thika Cloth Mills Limited (TCM), kuingilia kati na kuwasaidia wakulima wa Mpeketoni na Lamu kwa jumla.

Kiwanda hicho kwa sasa kimewekeza zaidi ya Sh36 milioni katia kuwanunulia na kuwasambazia bure bilashi wakulima wa kaunti ya Lamu mbegu za kisasa za pamba katika harakati za kupiga jeki kilimo hicho.

“Twawashukuru sana wahisani, hasa Thika Cloth Mills Limited. Wao wamekuwa wakinunua mbegu za kisasa za pamba na kugawia sisi wakulima. Pia wametupa soko wazi na la haraka, ambapo ndio wanaonunua pamba tunayokuza. Hili ni jambo linalowapa moyo wakulima wengi kujikita kwenye kilimo cha pamba miaka ya sasa,” akasema Bw Migwi.

Bi Susan Kariuki, mmoja wa wakulima wa pamba eneo la Baharini, tarafa ya Mpeketoni, pia alisifu juhudi zinazofanywa na serikali ya kaunti ya Lamu katika kukifufua kilimo cha pamba eneo hilo miaka ya hivi karibuni.

Kulingana na Bi Kariuki, kila mara serikali ya kaunti ya Lamu kupitia Gavana Issa Timamy, imekuwa ikisambazia wakulima mbegu za kisasa za pamba.

“Tulikuwa tumepoteza matumaini kwamba kilimo cha pamba kingefufuka. Twashukuru. Tuko na matumaini kwani wahisani wengi, ikiwemo serikali yetu ya kaunti, wamejitolea vilivyo kuunga mkono sekta ya pamba. Tuko na imani hali itarudi kama zamani,” akasema Bi Kariuki.

Bi Nancy Wangoi, mkulima wa pamba katika kijiji cha Salama, aliiomba kaunti kuzingatia kuwajengea kiwanda cha pamba Lamu ili iwe rahisi kwao kufikisha zao hilo katika soko linalofaa.

Bi Nancy Wangoi, ambaye ni mkulima wa pamba kijijini Salama, tarafa ya Mpeketoni, Lamu, avuna pamba kwenye shamba lake. Anaomba kiwanda cha pamba kijengwe maeneo yao ili kuwawezesha kuuza zao hilo karibu nao. PICHA | KALUME KAZUNGU

“Najua kiwanda cha pamba kikiwa papa hapa Lamu, wakulima wengi zaidi watavutiwa kukuza pamba. Soko pia litakuwa karibu nasi kuliko sasa,” akasema Bi Wangoi.

Kwa upande wake, Waziri wa Kilimo, Kaunti ya Lamu, Bw James Gichu alisema serikali ya kaunti inaendeleza mikakati kabambe ya kufaulisha kilimo cha pamba.

“Huku tukiendeleza majadiliano na mipango ya kujenga kiwanda cha pamba eneo hili, pia tumekuwa tukiendeleza juhudi za kununua na kusambazia wakulima wetu mbegu za kisasa za zao hilo. Lengo letu ni hadhi iliyokuwepo kuhusu pamba Lamu irejee,” akasema Bw Gichu.