Makala

Mpeketoni wataka kufutiwa vikumbusho vya shambulio la Al-Shabaab

April 28th, 2024 3 min read

NA KALUME KAZUNGU

NI miaka 10 imepita sasa huku macho ya wenyeji na wakazi wa Mpeketoni yakiendelea kuona magofu ya majumba na magari yaliyochomwa kwenye huo mji wakati wa shambulio la kigaidi mwaka 2014.

Bw Emmanuel Wanyoike Kimwa, ambaye ni mkazi na mfanyabiashara katika mji wa Mpeketoni anasema kila akiona magofu hayo, kinachomjia akilini mwake ni kuwa wapiganaji wa Al-Shabaab walimsambaratisha mwenye jengo au gari husika.

“Ni wajibu wa serikali yetu kutafuta mbinu za kusaidia hawa waathiriwa, ikiwa tunataka kufaulu kuondoa kabisa hizi kumbukumbu mbaya machoni mwetu,” anasema Bw Kimwa.

Mji huo unapatikana kaunti ndogo ya Lamu Magharibi.

Itakumbukwa kwamba mnamo Juni 15, 2014, magaidi wa Al-Shabaab walivamia mji huo na kuua watu wapatao 90 kwa usiku mmoja.

Vijana wawili wakitazama majina ya watu waliouawa kwenye shambulio la kigaidi la Juni 15, 2014 mjini Mpeketoni. Zaidi ya watu 90 walioawa mjini humo kwa usiku mmoja. PICHA | KALUME KAZUNGU

Nyumba zaidi ya 30 na magari karibu 40 yalichomwa na kuharibiwa na magaidi wa kutoka nchi jirani ya Somalia wakati wa shambulio hilo lililotekelezwa usiku, hali iliyouacha mji wa Mpeketoni ukiwa.

Karibu mwongo mmoja ukiwa umepita sasa aidha, mji wa Mpeketoni unaendelea kupata sura mpya kwani majengo mapya yamechipuka ilhali mengi ya yale yaliyoteketezwa yakikarabatiwa na kupewa mwonekano wa kuvutia.

Licha ya maendeleo hayo kujiri, bado kumekuwa na vilio miongoni mwa wenyeji wa Mpeketoni kuhusiana na makovu ambayo bado yanapatika mahalimahali mjini humo.

Bi Tabitha Kamau anasisitiza kuwa kumbukumbu za tukio baya la kigaidi la 2014 mjini Mpeketoni zitazikwa katika kaburi la sahau iwapo mabaki yote, ikiwemo yale ya magari na majumba yaliyochomwa yataondolewa au kubadilishwa mwonekano.

“Fikra za shambulio la 2014 hapa Mpeketoni zitafutika vipi akilini ikiwa ukipinda shingo huku waona mabaki ya magari yaliyochomwa na kwingine mabanda ya nyumba zilizochomwa? Serikali ije na mfumo wa kuwasaidia walioharibiwa hizi mali zao kurejelea hali yao ya kawaida na mabaki yaondolewe au kubomolewa mjini,” akasema Bi Kamau.

Samuel Wachira naye anasema huku serikali ikisubiriwa kushughulikia waathiriwa wa ugaidi Mpeketoni, ipo haja ya njia ya haraka kufanywa kuziondoa kumbukumbu mbaya kwenye mazingira ya wanaoishi Mpeketoni.

Kimojawapo cha vituo vya mafuta mjini Mpeketoni ambacho kiliteketezwa na Al-Shabaab lakini kwa sasa kimepewa sura mpya, hivyo kufuta kumbukumbu mbaya. PICHA | KALUME KAZUNGU

Bw Wachira anapendekeza mfumo wa mabaki ya majumba au magari yaliyounguzwa na Al-Shabaab kupigwa rangi ya samawati au nyeupe iliyokoleza.

“Tukisubiri serikali kufidia waathiriwa wa ugaidi Mpeketoni tutachoka. Tumekuwa tukisukumana na serikali hiyo hiyo tangu 2014. Waathiriwa hata walikuwa wameahidiwa kwamba wangejengewa hizi nyumba lakini wapi. Hakuna lililotimizwa. Cha msingi ni kutumia njia za haraka, ikiwemo kupiga rangi haya magofu ya Al-Shabaab na mabaki yote ya magari yaliyochomwa. Mwonekano wa sasa ni wa kukera na kutisha,” akasema Bw Wachira.

Kwa upande wake, Bi Mary Kananu alisema kuendelea kuwepo kwa mabaki ya nyumba na magari yaliyochomwa na Al-Shabaab ni sawa na kulitutukuza tukio hilo la shambulio la kigaidi.

Bi Kananu aliwashukuru wengi wa wanajamii wa Mpeketoni kwa kuondoa woga, kuupiga moyo konde na kuendelea kujijenga licha ya hasara waliyokadiria wakati wa uvamizi wa kigaidi wa 2014.

“Nafurahia vile wenzangu hapa Mpeketoni hawakutishwa na tukio la kigaidi la 2014. Kila mmoja yuko mbioni kujijenga. Mpeketoni inazidi kukua, hivyo kurejelea hadhi yake ya zamani na hata kushuhudia maendeleo mengine zaidi,” akasema Bi Kananu.

“Na ndio sababu twafaa kufuta kumbukumbu zote mbaya zilizoko mjini hapa, ikiwemo haya mabaki ya magari, pikipiki na majumba yote yaliyochomwa. Kuendelea kuishi nayo hapa ni sawasawa na kutukuza ugaidi ambao kikweli tumeushinda,” aliongeza.

Mbali na Mpeketoni, maeneo mengine ya Lamu ambayo yameshuhudia uvamizi na mauaji ya Al-Shabaab ni Kibaoni, Witu, Hindi, msitu wa Boni na viunga vyake.

Mnamo Septemba 2015, serikali kuu ilizindua operesheni ya Kiusalama kwa jina ‘Linda Boni’ dhamira kuu ikiwa ni kuwasaka na kuwamaliza magaidi wa Al-Shabaab wanaoaminika kujificha ndani ya msitu mkuu wa Boni.

Operesheni hiyo aidha imekuwa ikibadilishwa majina kila wakati kutoka Linda Boni, Boni Enclave Campaign, Operesheni Fagia Msitu na kwa sasa Operesheni Amani Boni (OAB).

Inatekelezwa na vitengo mbalimbali vya usalama chini ya uongozi wa Jeshi la Ulinzi Kenya (KDF).

Vitengo vingine ni Polisi (NPS), Shirika la Huduma kwa Wanyamapori (KWS), lile la Huduma za Misitu (KFS), Vijana wa Huduma kwa Taifa (NYS), maafisa wa utawala wa kitaifa (NGAO) na wengineo.

Tangu operesheni hiyo kuanzishwa, Lamu imeshuhudia kuimarika pakubwa kwa hali ya usalama, ambapo visa vya Al-Shabaab kuvamia na kuuawa wananchi na walinda usalama vimepungua pakubwa.