Habari Mseto

Mpelelezi motoni kutisha kuua washukiwa aliokuwa akichunguza

September 18th, 2019 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MCHUNGUZI wa kibinafsi Jane Mugoh alishtakiwa Jumatano kwa kutisha kuwaua washukiwa wawili aliokuwa anawachunguza.

Huku Bi Mugoh akishtakiwa mahakamani waandamanaji wakiwa na mabango walisimama nje ya mahakama” wakiomba aachiliwe na wanaodhulumu wakome.”

Bi Mugo alikana mashtaka dhidi yake aliposhtakiwa mbele ya hakimu mkuu Francis Andayi.

Bi Mugo alikabiliwa na shtaka la kutisha kumuua Deepak Shah mnamo Februari 2, 2019 katika mtaa wa Kyuna kaunti ya Nairobi.

Shtaka lilisema Bi Mugo alimtisha Bw Shah kwa kumchomolea bastola na kutisha kumfyatulia risasi.

Shtaka la pili lilisema mnamo Agosti 15 2019 katika mtaa wa New Muthaiga alimtisha kumuua Patrick Mugasia Kefa kwa bastola.

Kiongozi wa mashtaka Angela Fuchaka aliomba mshtakiwa apelekwe kwa msajili wa silaha katika afisi ya Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Jinai ndipo silaha hiyo ikaguliwe.

Wakili Dunstan Omari anayemwakilisha aliomba aachiliwe kwa dhamana.

“Mshtakiwa hawezi kutoroka. Ni mzazi na yuko na watoto anaowatunza,” alisema Bw Omari

Aliomba aruhusiwe kumpeleka mshtakiwa kwa DCI Alhamisi kwa vile alikuwa anahudhuria zoezi la kufanyiwa upasuaji maiti ya mfanyabiashara bilionea Tob Cohen aliyetoweka Julai 19/20 na maiti yake ikapatikana imetupwa kwa tangi la maji taka.