Shangazi Akujibu

Mpenzi hanipi pesa, zote zaenda kwa mamake, nishauri

May 16th, 2024 1 min read

Vipi shangazi. Nimekuwa katika uhusiano wa kimapenzi na kaka huyu kwa zaidi ya miaka miwili sasa. Bwana huyu amekataa kabisa kunishughulikia kifedha, ilhali anakidhi mahitaji ya mamake. Nimteme?

Ni upumbavu kulinganisha umuhimu wako katika maisha ya kaka huyu, na ule wa mamake mzazi. Hata hajakuoa na tayari unataka mahitaji yako ya kifedha yashughulikiwe? Tafuta ajira binti!

Mume wangu anavunda nguo za ndani

Mpendwa shangazi. Tumeoana na mume wangu kwa miaka miwili sasa na tayari ameanza kunichosha. Kinachoniudhi kumuhusu ni kwamba mwanamume huyu ni mchafu kupindukia, kiasi cha kwamba hata nguo zake za ndani zinavunda. Wakati wa mahaba inanibidi nivalie barakoa. Nitamfanyaje?

Bila shaka kila mtu ana wajibu wa kudumisha usafi wa mwili wake, lakini kama mke, pia wewe una jukumu la kumng’arisha mumeo. Mwambie ukweli lakini pia wewe msaidie.

Wazazi wanamtafutia mume mwingine

Za masiku shangazi? Kwa miaka minne nimekuwa nikiishi na binti huyu ambaye naamini ni mke wangu, japo bado sijamtolea mahari wala kumuoa rasmi. Hata tuna mtoto mmoja. Lakini, hivi majuzi niligundua wazazi wake wamekuwa wakimtafutia mume mwingine eti mimi ni fukara. Naomba usaidizi.

Uhusiano wenu ni baina ya watu wawili, na hivyo jamaa zake hawapaswi kuingilia masuala yenu, hasa ikiwa mnaishi kwa amani. Lakini pia wewe unapaswa kuchangamka. Utaishije na binti ya mtu muda huu wote bila kurasmisha mambo?

Mke ana mume mwingine

Shangazi. Wiki kadhaa zilizopita niligundua kwamba mke wangu wa miaka kumi ana mume mwingine. Hii ni baada ya kukumbana na hati ya ndoa baina yake na huyu mwanamume, nyumbani mwetu. Kinachostaajabisha hata zaidi ni kwamba walioana tukiwa katika hii ndoa yetu. Moyo unauma.

Suluhisho ni kumuuliza mkeo waziwazi kuhusu hati hii uliyokumbana nayo. Baada ya hapo itakuwa rahisi kufanya uamuzi wa busara.