Habari Mseto

Mpigambizi Mswidi ashindwa kupata miili ya Kighenda na mwanawe

October 5th, 2019 1 min read

Na CHARLES WASONGA

MPIGAMBIZI kutoka raia wa Uswidi, Volter Bassen mnamo Ijumaa jioni aliyafifisha matumaini ya familia ya Miriam Kighenda baada ya kufeli kupata na kuopoa mwili waka na wa bintiye, Amanda Mutheu, kutoka Bahari Hindi.

Familia hiyo ilikuwa na matumaini kwamba msako wa maiti za wapendwa wao ambao Ijumaa ilifikia siku ya tano, ungekamilika baada ya Bassen kuahidi Alhamisi kwamba angepata na kuopoa miili hiyo kwa muda wa saa mbili.

Mswidi huyo ambaye ameoa Mkenya, amekuwa akiishi nchini tangu miaka ya tisini (1990s).

Alikuwa mmoja wa wapigambizi 16 wanaoendesha juhudi za kuopoa miili za Bi Kighenda na bintiye waliokufa maji katika kivuko cha Likoni.

“Niligundua kuwa ukadiriaji wangu kuhusu hali hapa haukuwa sahihi,” akasema Bassen ambaye aliongea na wanahabari mwendo wa saa 12 na dakika 45 Ijumaa.

Alikuwa ameandamana na Msemaji wa Serikali Kanali mstaafu Cyrus Oguna, watu wa familia ya Kighenda na wanachama kadhaa wa kikosi kinachoendesha shughuli ya uokoaji.

Oguna alisema wapigambizi 16 walikuwa katika sehemu tatu ambazo walikuwa wametambua kwamba huenda gari la Bi Kighenda lingepatikana.

“Mpaka sasa japo tungali na matumaini, hatuhafaulu,” msemaji wa serikali akasema.

Hata hivyo, Kanali Oguna alisema shughuli za uokoaji na uopoaji hazitakomeshwa.

“Tutatumia mitambo mbalimbali kuendeleza msako na ukusanyaji wa data zaidi,” akasema.

Bw Bassen alisema ni vigumu kuona kitu ndani ya maji, hali inayofanya operesheni ya uokoaji kuwa ngumu.

“Maji ya hapa ni ya kina kirefu, na kuna mawimbi makali ya chini mwa chini; hali inayolemea juhudi zetu za kupata mabaki ya gari hili,” Mswidi huyo akasema.