Mpinzani mkuu wa Kagame akamatwa kwa dai la unajisi

Mpinzani mkuu wa Kagame akamatwa kwa dai la unajisi

Na MASHIRIKA

KIGALI, RWANDA

MHADHIRI wa chuo kikuu nchini Rwanda ambaye ni kiongozi wa upinzani, Alhamisi alikamatwa kwa madai ya unajisi, polisi walisema.

Christopher Kayumba anakabiliwa na madai kutoka kwa watu kadhaa akiwemo mwanafunzi wake wa zamani, ilisema taarifa ya uchunguzi wa jinai nchini Rwanda (RIB).

“Leo, RIB ilimkamata Dkt Christopher Kayumba baada ya kumchunguza kwa muda kufuatia madai ya kutisha na kunajisi yaliyoripotiwa na watu kadhaa,” ilisema taarifa ya RIB.

Taarifa hiyo iliongeza kuwa kesi yake ilikuwa imewasilishwa kwa waendesha mashtaka.

Kayumba, 48, anaendesha gazeti la mtandaoni linaloitwa ‘The Chronicles’ na mnamo Machi aliunda chama cha kisiasa kumpinga Rais Paul Kagame.

Punde baada ya kuunda chama hicho, madai ya unajisi yaliibuka kwenye mitandao ya kijamii na akayakanusha.

Mnamo Desemba 2019, Kayumba alihukumiwa kifungo cha mwaka mmoja kwa kuzua vurugu baada ya walinzi katika uwanja wa ndege kumzuia kusafiri hadi Nairobi.

Maafisa walisema kwamba alifika katika uwanja huo akiwa amechelewa na mlevi na kutisha kufunga uwanja huo.

Mnamo Juni, mhadhiri mwingine wa chuo kikuu Aimable Karasira, aliyemlaumu Kagame kwenye YouTube, alishtakiwa na angali kizuizini.

Karasira, aliyenusurika mauaji ya halaiki ya 1994 nchini Rwanda ambapo watu 800,000 waliuawa, anadai kwamba chama tawala cha Rwandan Patriotic Front kiliua wazazi wake.

You can share this post!

Laikipia yalipia makosa ya Wakoloni

Hatari Afrika ikipunguziwa chanjo ya corona hadi nusu