Mpira wa Vikapu: Kenya yaambulia patupu mashindano ya Red Bull Half Court

Mpira wa Vikapu: Kenya yaambulia patupu mashindano ya Red Bull Half Court

NA RUTH AREGE

KENYA ilibanduliwa mapema kwenye makala ya pili ya mashindano ya dunia ya mpira wa vikapu ya Red Bull Half Court ya wachezaji watatu kila upande (3×3) ambayo yalikamilika Cairo nchini Misri wikendi.

Timu zote nne zilitemwa mapema kwenye hatua ya makundi. Timu hizo ni pamoja na timu za wanawake za Elite na Dynamites ya Chuo Kikuu cha Nairobi (UON). Wanaume  waliwakilishwa na Nameless na Kenya One.

Makala ya kwanza ambayo yalifanyika Roma nchini Italia mwaka 2021, Kenya haikuwa na mwakilishi kutokana na mlipuko wa Covid-19. Timu mbili ambazo hazikuweza kusafiri wakati huo zilijumuishwa kwenye makala ya mwaka huu.

Timu ya Elite pamoja na Kenya One walikuwa mabingwa mwaka huu nao Dynamites na Nameless walitwaa ubingwa mwaka 2021.

Kenya One wakatapata ushindi mmoja dhidi ya Uswizi kwa alama 16-15 na wakapoteza mechi mbili dhidi ya Australia, Czech Repulic na Italia. Nao Nameless wakarushwa kundi moja na Serbia ambao walikuwa mabingwa watetezi, Maldavies, United Arabs Emirates na Great Britain.

Nameless waliandikisha ushindi wa mechi moja na kupoteza mbili. Walipata ushindi wa kwanza kwa alama 8-1 dhidi ya Maldavies, walipoteza kwa alama 7-8 na 8-9 dhidi ya Serbia na United Arabs mtawalia.

Elite ambao walipangwa kundi moja na Australia na Uswizi walipoteza mechi zote. Kwenye mechi ya mwisho ya hatua ya makundi walipoteza dhidi ya mabingwa watetezi Australia kwenye hatua ya makundi kwa alama 9-7.

Dynamites ilikuwa ni timu ya pekee kutoka Kenya kujikatia tiketi ya kuingia kwenye robo fainali ya mashindano hayo. Kwenye mechi ya kwanza, waliwanyuka Uturiki alama 6-3. Walipoteza mechi mbili dhidi ya Italia na Jordan.

Stellah Nekesa ambaye aliwakilisha Elite alikiri kuwa, mashindano kama haya yanawapa nafasi ya kuonyesha talanta zao na pia kujifunza kutoka kwa mataifa mengine.

“Tulikuwa watatu tu kutoka Kenya, na mshindano yalikuwa mazuri. Tulicheza mechi tatu lakini hatukufanikiwa kushinda hata moja. Si kwamba kikosi chetu kilikuwa kibaya, tulijaribu tuwezalo,” alisema Nekesa.

Kwa upande wa mchezaji wa Kenya one Fredrick Onono alisema, kucheza kwenye mashindano hayo ni njia mojawapo ya kupata mafunzo zaidi ya kucheza wa mpira wa vikapu.

“Hali ya anga ilikuwa ya joto sana, lakini tumejifunza mengi kutoka kwa mashindano haya na tukirudi nyumbani tutawafunza na wenzetu. Wapinzani walikuwa wanatoka nchi ambazo zinatamba sana mpira wa vikapu duniani. Hili ni jambo nzuri na tunatazamia mashindano kama haya siku zijazo,” alisema Onono.

Mchezaji wa klabu ya Nameless Martin Kibet alikiri kuwa, mbinu ambazo Kenya inatumia kucheza ni tofauti na mataifa mengine.

“Tumejifunza jinsi ya kufanya maandalazi kabla ya kila mashindano. Tukirudi nyumbani tutarekebisha makosa kama ya kushambulia na pia kuzuia. Huu ni mchezo ambao unakua Kenya ¬†siku za hivi karibuni, siku zijazo Kenya itatamba Afrika. Ilikuwa mara yetu ya kwanza kucheza mashindano ya kimataifa tulifanya vizuri,” aliongezea Kibet.

  • Tags

You can share this post!

Kibarua cha Raila kulinda ufuasi Gusii

TAHARIRI: Visasi na chuki ni vikwazo kwa nchi kuendelea

T L