Bambika

Mr Seed akomoana na mkewe mtandaoni kwa kusema ‘mwanamume ni wa wanawake wengi’

January 25th, 2024 1 min read

NA FRIDAH OKACHI

MWANAMUZIKI wa nyimbo za Injili Moses Tarus Omondi almaarufu ‘Mr Seed’ ameomba msamaha kwa mkewe Nimo baada ya kunukuliwa kwenye podcast akitoa kauli tata.

Kwenye ukurasa wake wa Instagram, Mr Seed aliomba msamaha kwa matamshi yake yaliyojikita kwa mtazamo wake kuhusu ndoa.

Kwenye mahojiano hayo, alisema kwamba ni kawaida wanaume kuvutiwa na hata kutekwa kihisia na wanawake wengi.

Alienda hatua zaidi kusema mwanamke kuishi naye kwa muda mrefu si kigezo cha kumfanya kuhisi kwamba ameshinda kwani anaweza kuamka siku moja agundue mume wake anapanga kufunga harusi na mwanamke mwingine.

Matamshi hayo yalionekana kumuudhi mkewe Nimo ambaye kupitia Instastory zake, alimkemea vikali akidai kuwa maneno hayo hayakufaa kutoka kwa kinywa cha mwanamume anayejua kwamba yuko katika ndoa imara.

Lakini sasa mwimbaji huyo amebainisha kwamba hakukusudia kumuumiza mkewe na kuahidi mke wake kwamba atabadilika.

“Mpendwa naomba msamaha kwa maudhi ambayo sikukusudia. Matamshi yangu ya hivi majuzi kuhusu ndoa na zaidi, ndoa ya mitara yanaweza kuwa yamesababisha kero,” alisema Mr Seed.

“Natambua sasa maneno yangu hayakuendana na heshima niliyo nayo kwako. Hisia zako ni muhimu sana kwangu, na nimejitolea kuwa mwenye kufikiria zaidi katika mazungumzo yangu kusonga mbele,” aliongeza.

Mwanamuziki huyo alizungumzia masuala ya mahusiano ambapo alisema kwa tajriba yake kwenye ndoa, mwanamume ni kiumbe ambaye anaweza akawa kwenye mahusiano na mwanamke kwa miaka mitatu lakini bado akawa anawazia kuoa mwanamke mwingine.

Mkewe Mr Seed, siku ya Jumatano aliacha kumfuata kwenye mitandao ya kijamii.