Habari Mseto

Mradi wa barabara Juja wakwama ghafla

July 17th, 2019 1 min read

Na LAWRENCE ONGARO

WAKAZI wa eneo la Juja Farm katika Kaunti ya Kiambu, wanalalamika baada ya mradi wa ujenzi wa barabara kukwama.

Barabara ya urefu wa kilomita 12 ambayo ilizinduliwa majuzi na Gavana Ferdinand Waititu sasa imebaki tu na mafungu ya udongo uliokusanywa na hivyo kutatiza usafiri.

Msingi ulioashiria ujenzi wa barabara eneo la Juja Farm. Picha/ Lawrence Ongaro

Bw Francis Mwangi, mhudumu wa bodaboda, alisema Jumanne barabara hiyo ya Juja Centre hadi Juja Farm, imekwama baada ya mwananchi wa kawaida kupata ya kwamba ukarabati wake ulisitishwa.

“Katika siku za hivi karibuni tumegundua ya kwamba matingatinga ya kuchimba udongo yaliyokuwa huku yameondolewa na hatujui yalikopelekwa,” alisema Bw Mwangi aliyeongeza kwamba udongo katika sehemu hiyo ya barabara ni wa matope.

Alisema wanatumia pesa nyingi kurekebisha pikipiki zao kutokana na kuvunjika kwa vyuma.

Bw John Wamui ambaye ni mkazi wa kijiji cha Juja Farm alisema matingatinga yaliyokuwa yakiendesha ukarabati wa barabara hiyo tayari yameondolewa na kupelekwa kusikojulikana.

“Sisi wakazi wa hapa tuna shida; katika barabara hii kumeachwa rundo la mchanga ambalo ni tatizo kwa wahudumu wa matatu,” alisema Bw Wamui.

Mashimo wazi

Naye Bi Sarah Wambui Chege, alisema wakazi wa Juja Farm wanapitia masaibu mengine kwenye barabara hiyo.

“Wakati wa uzinduzi wa barabara hiyo tulifurahia mpango huo lakini sasa mashimo yaliyochimbwa yamekuwa ni habari kwa usalama kwa kuachwa wazi bila kuyaziba,” alisema Bi Chege.

Mradi huo wa barabara umeendeshwa kwa mwezi mmoja na nusu pekee kabla ya kusitishwa, kulingana na maelezo ya Bi Chege.

Wakazi hao walielezea waandishi wa habari kuwa juhudi zao za kufuatilia jambo hilo kupitia afisa ya Gavana Ferdinand Waititu, zimegonga ukuta kwa sababu hakuna yeyote aliye tayari kufafanua kinachoendelea.

Juhudi za kutafuta maafisa wa wizara ya barabara na ujenzi katika kaunti ya Kiambu hazikufua dafu kwani hakuna yeyote alikuwa tayari kuelezea lolote kuhusu madai hayo.