Habari

Mradi wa bwawa Kariminu wang'oa nanga

August 8th, 2019 1 min read

Na LAWRENCE ONGARO

MRADI mkubwa wa maji wa Kariminu II Dam wa kiasi cha Sh24 bilioni katika maeneo ya Buchana, Kiriko, Gathanji na Kanyoni tayari umeanza kuchimbwa.

Matingatinga yalifika katika maeneo hayo mwishoni mwa wiki jana ambapo kufikia sasa kazi inaonekana ikiendelea kwa kasi.

Wakazi wa sehemu ya kwanza ya Kariminu I Dam walilipwa fidia zao huku wale wa sehemu ya pili wakiwa wanakaribia kukamilishiwa haki yao.

Mbunge wa Gatundu Kaskazini Bi Wanjiku Kibe tayari amewahakikishia wakazi hao wawe na subira huku matakwa yao yakishughulikiwa haraka iwezekanavyo.

“Ninawahimiza wakazi wa hapa wawe na subira kwani serikali iko mbioni kuona ya kwamba kila mkazi anapokea haki yake bila kuchelewa,” akasema Bi Kibe.

Wakazi wa Kanyoni na Gathanje wanaitaka serikali iharakishe fidia katika kikundi cha pili kwa sababu wanataka kujitafutia ardhi kwingineko.

“Sisi wakazi wa sehemu hizi tunahofia pengine fedha zetu zinaweza kucheleweshwa kulipwa. Tunamuomba mbunge wetu afanye juhudi kuona ya kwamba tunapata haki yetu mara moja,” alisema Bw Jackson Mbugua ambaye ni mkazi wa Gathanje.

Hivi majuzi Waziri wa Maji Bw Simon Chelungui alizuru sehemu hiyo na kujionea mwenyewe jinsi kazi hiyo ilivyotarajiwa kuzinduliwa rasmi.

Sehemu ya kwanza ya eneo hilo ni ya ekari 171.6 ambako zinatoka familia 246. Tayari zimeshapokea takribani Sh1.28 bilioni kama fidia.

Kulingana na wahandisi wa mradi huo, bwawa hilo ni la futi 59 na linatarajiwa kusambaza maji mengi kwa takribani watu milioni moja.

Kulingana na mipango ya utekelezwaji, mradi wenyewe utachukua muda wa miezi 48 kukamilika. Litakamilika mwaka wa 2023.

Maji ya bwawa hilo yatasambazwa katika maeneo ya Ruiru, Thika, Juja, Gatundu Kaskazini, na baadhi ya mitaa ya jiji kuu Nairobi.

Mradi huo pia unafadhiliwa na serikali ya Kenya na China Exim Bank kwa ushirikiano na kampuni ya International Holding Corporation na Shangai Municipal Engineering Design Institute.