Habari Mseto

Mradi wa bwawa la maji wa Karimenu Phase 11 waendelea Gatundu Kaskazini

September 27th, 2019 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

MRADI wa bwawa la maji wa Karimenu Phase 11 Gatundu Kaskazini umezinduliwa huku serikali ikitenga kitita cha fedha za kuwalipa fidia wakazi wa eneo la mradi huo ambao wataathirika.

Waziri wa Maji, Simon Chelugui, alisema tayari Sh2 bilioni zimetengwa kuwalipa wakazi hao ili wahame kutoka pahala hapo pa mradi.

“Kwa wakati huu serikali haina fedha za kutosha lakini imetenga Sh1 bilioni zitakazotolewa huku ikisalia na Sh1.2 bilioni ili kukamilisha deni hilo,” alisema waziri Chelugui.

Aliahidi kwamba wizara yake itafanya juhudi kuona ya kwamba ajenda nne kuu za serikali zinatekelezwa ipasavyo.

“Mradi huo utafuatiliwa kwa makini ambapo unatarajiwa kukamilika ifikapo Juni 2022. Kwa hivyo, wahandisi wanaoendesha mradi huo wanastahili kuharakisha kazi hiyo ili iweze kukamilika,” alisema Bw Chelugui.

Waziri wa Maji Bw Simon Chelugui (wa pili kushoto akiwa amevalia kofia nyeupe) akiandamana na Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang’i katika mradi wa Karimenu Phase II Septemba 26, 2019. Picha/ Lawrence Ongaro

Alisema Sh10 bilioni zitatengwa ili kufanikisha miradi ya maji katika maeneo ya Kiambu, Limuru na Kikuyu.

“Tunataka kuona ya kwamba katika maeneo hayo yote kumesambazwa maji ili wananchi wanufaike na maji safi,” alifafanua waziri huyo.

Waziri wa usalama ya ndani Dkt Fred Matiang’i ambaye alizuru pia mradi wa maji wa Karimenu, alisema machifu washirikiane na familia za eneo hilo ili kutatua maswala ya urithi wa mashamba.

“Iwapo hali ya urithi litatatuliwa haraka bila shaka hata mambo ya malipo ya fidia itakamilika haraka bila mvutano,” alisema Dkt Matiang’i.

Mbunge wa Gatundu Kaskazini Bi Wanjiku Kibe, alisema wakazi wa eneo hilo la Karimenu watapata fidia ili waende kuishi eneo mbadala.

“Tunataka kuona mradi huo ukiendeshwa kwa njia ifaayo bila kunyanyasa na kuhujumu yeyote. Ningetaka kuona wahandisi wanaoendesha mradi huu kuona ya kwamba vijana wetu wa eneo hili wanapata ajira kwa njia moja ama nyingine,” alisema Bi Kibe.

“Wakazi wa eneo hili wanastahili kupewa kandarasi ya kuuza vifaa vya ujenzi na kusafirisha saruji na mchanga katika eneo la mradi. Hii itakuwa njia moja ya kubuni ajira kwa wakazi wa hapa eneo langu la uwakilishi,” alisema Bi Kibe.

Mwakilishi wa Wanawake wa Kaunti ya Kiambu katika Bunge la Kitaifa, Bi Gathoni Wa Muchomba, alipendekeza wafanyakazi katika mradi huo wapewe mafunzo rasmi ili waweze kurekebisha mitambo hiyo iliyopo mahali hapo. Hi ni kwa sababu wakati wahandisi wa kutoka wa China watakaporejea makwao wakazi wa hapa watakuwa wajuzi wa kurekebisha mashine hizo.

“Sisi viongozi wa eneo hili la Kiambu tunafuata ajenda nne muhimu zinazopendekezwa na Rais wetu Uhuru Kenyatta. Tukifanya hivyo bila shaka tutaafikia malengo hayo,” alisema Bi Muchomba.

Mbunge wa Gatundu Kusini Bw Moses Kuria alipongeza juhudi za serikali kuunda barabara Gatundu.

“Kwa muda wa miaka michache sasa tumeona maendeleo katika kila sehemu ambapo maji na hata umeme umesambazwa kila eneo. Kwa hivyo ni lazima tuipongeze serikali yetu kwa kazi hiyo nzuri,” akasema Kuria.

Naibu gavana wa Kiambu Bw James Nyoro alisema kiwanda cha kutengeneza matunda kitajengwa eneo la Gatundu Kaskazini ili kiweze kuajiri vijana wengi.

Alipendekeza pia msitu wa Kinari uhifadhiwe kwa lengo la kuhifadhi mazingira kwa njia ifaayo.

“Tunataka kuona ya kwamba msitu huo unahifadhiwa kwa njia inayostahili ili kulinda hali ya mazingira,” alisema Bw Nyoro.