Habari za Kaunti

Mradi wa Dongo Kundu kuendelea baada ya muafaka

March 26th, 2024 1 min read

NA ANTHONY KITIMO

MIEZI mitano baada ya Rais William Ruto kusimamisha ulipaji wa fidia ya Sh1.4 bilioni kwa walioathiriwa na mradi wa kibiashara wa Special Economic Zone (SEZ) wa Dongo Kundu, serikali imeweka mikakati ya kufufua mradi huo.

Zaidi ya wakazi 1,648 kutoka eneo la Dongo Kundu, Mwangala, Mrongondoni, Kaya Mtongwe, Mbuta na Siji wanatarajiwa kuachia serikali ardhi ya zaidi ya ekari 357 kuendeleza mradi huo wa SEZ baada ya serikali kutatua matatizo yaliyokuwa kizingiti kuwafidia.

Katibu katika Idara ya Uwezeshaji wa Uwekezaji katika Wizara ya Uwekezaji, Biashara na Ustawi wa Viwanda Abubakar Hassan amesema matatizo yote ya kufidia wakazi yametatuliwa na watapokea pesa zao chini ya miezi miwili ijayo.

“Rais Ruto aliagiza tutekeleze mradi huu kwa haraka na matatizo yote ya fidia yamekamilika hivyo basi pesa hizo zitatolewa ama Aprili au Mei ili kuhamisha watakaoathirika na mradi. Fedha hizo zitalipwa na kupitia Halmashauri ya Bandari nchini (KPA) baada ya Tume ya Ardhi Nchini (NLC) kukamilisha ukaguzi,” alisema Bw Hassan.

Akiongea katika makao makuu ya bandari ya Mombasa baada ya mkutano na washikadau wa mradi huo, katibu huyo alisema punde tu baada ya kulipa waliokuwa katika ardhi hizo, serikali itatoa maombi kwa wale wote wanaonuia kuwekeza katika eneo hilo kutuma stakabadhi zao.

“Kwa sasa ni wawekezaji watatu pekee ambao wako katika eneo hilo ikilinganishwa na 16 eneo la Naivasha. Tunajua tatizo la ardhi ndilo limesababisha kuchelewa kwa wawekezaji lakini hilo tumelitatua,” alisema katibu huyo.