Habari Mseto

Mradi wa kufufua reli inayounganisha Nairobi na Nanyuki wakaribia kukamilika

June 12th, 2020 2 min read

SAMMY WAWERU na LAWRENCE ONGARO

MRADI wa kufufua reli inayounganisha Nairobi na Nanyuki unakaribia kukamilika ikitarajiwa usafiri wa treni utakuwa ni afueni kwa wenye viwanda, wafanyabiashara na wananchi kwa jumla.

Waziri wa Uchukuzi James Macharia amesema Ijumaa ujenzi wa reli hiyo iliyoasisiwa wakati wa serikali ya mkoloni, umefikia asilimia 90.

“Kufikia sasa shughuli za ujenzi zimefika asilimia 90, na hivi karibuni utakamilika,” waziri Macharia amesema.

Hata ingawa hajasema wazi muda rasmi ambao mradi huo utakamilika, waziri huyo amesema wakandarasi waliopewa jukumu kuushughulikia wanafanya juhudi kuhakikisha reli hiyo imeimarika.

Kando na kurahisisha shughuli za usafiri kati ya jiji la Nairobi na Nanyuki, na maeneo yaliyo kati, Bw Macharia amesema reli hiyo itakayotumia treni za kisasa pia itasaidia katika usafirishaji wa mizigo.

Mbunge wa Thika Bw Patrick ‘Jungle’ Wainaina amesema ufunguzi wa safari ya treni kutoka Nairobi hadi Nanyuki utakuwa wa manufaa kwa wafanyabiashara wengi.

“Ninatarajia mpango huo utakapokamilika rasmi mizigo itasafirishwa salama hadi kwenye bandari ya Mombasa. Usafiri wa barabara una mahitaji mengi ya ukaguzi huku reli ikiwa njia bora zaidi,” amesema Bw Wainaina.

Amesema reli ya kutoka Nairobi hadi Nanyuki itakuwa na manufaa kubwa kuliko awali lakini kwa zaidi ya miaka 15 imekuwa haitumiki.

“Wakati huu hata wananchi watapata afueni kusafiri kwa garimoshi kutoka Nairobi hadi Nanyuki,” amesema Bw Wainaina.

Meneja wa shughuli za uchukuzi wa Shirika la Reli Nchini (KR) Bw James Siere amesema ukarabati wa reli kutoka Jijini Nairobi hadi Nanyuki imekamilika kwa asilimia 80 huku mahali paliposalia ni asilimia ndogo sana.

“Tunatarajia ifikapo mwishoni mwa mwezi Juni 2020, kazi hiyo itakuwa imefika kikomo na uchukuzi wa mizigo utaanza rasmi,” amesema Bw Siere.

Ameeleza kwamba imechukua muda mrefu kazi hiyo kukamilika kwa sababu vyuma vya reli vilivyokuwepo vilikuwa na kutu na ilibidi vingine vipya viwekwe.

“Tuna matumaini katika miezi michache ijayo uchukuzi wa mizigo utang’oa nanga,” amesema meneja huyo.

Amewahimiza wafanyabiashara wajitokeze kwa wingi kutumia uchukuzi wa reli.

Amesema wahandisi wakuu watalazimika kuchunguza maeneo yote kama yako sawa ili kuruhusu mabehewa ya mizigo kuanza kazi.

Meneja wa uzalishaji wa matunda katika kiwanda cha Delmonte Bw Wayne Cook, amesema uchukuzi wa treni utakuwa wa manufaa kwao kwa sababu shehena za matunda zitachukuliwa mjini Thika hadi Mombasa bila shida yoyote.

“Tukianza uchukuzi wa kusafirisha shehena zetu za matunda tunatarajia kazi itakuwa rahisi ambapo mizigo hiyo itasafirishwa moja kwa moja hadi bandari la Mombasa. Hiyo itapunguza kuharibika kwa matunda njiani,” amesema Bw Cook.

Amesema usafiri wa barabara ulikuwa na matatizo mengi hasa ya kukaguliwa kila mara na maafisa wa usalama huku wakiulizia stakabadhi za shehena hizo.

Amezidi kueleza ya kwamba kampuni ya Delmonte itanufaika pakubwa kwa sababu watakuwa na imani ya kwamba mizigo yao itasafirishwa nchi za nje kwa utaratibu unaofaa bila matata.

Wiki jana, wafanyabiashara waliojenga vibanda kandokando mwa reli hiyo eneo la Karatina, walifurushwa huku vibanda vyao vikibomolewa ili kuruhusu ujenzi kufanyika.

Ni hatua iliyokosolewa na mbunge wa Mathira Rigathi Gachagua, akisema ubomoaji huo haukupaswa kufanywa wakati huu wafanyabiashara wanaendelea kulemewa na athari za janga la Covid-19.

Shirika la Reli la Kenya, KRC hata hivyo lilikuwa limetoa notisi ya ubomozi mapema mwaka huu.

Wafanyabiashara walioathirika walidai eneo walilotengewa halitoshi kusitiri zaidi ya wafanyabiashara wapatao 2,000 waliosukumia gurudumu la maisha kandokando mwa reli Karatina.

Aprili 2020 wafanyabiashara wa Chaka, Nyeri, waliokuwa wakiuzia bidhaa kandokando mwa reli waliondolewa ili kuruhusu ujenzi kufanyika.

Ufufuaji wa reli hiyo yenye urefu wa kilomita 240 unagharimu kima cha Sh3 bilioni.