Habari Mseto

Mradi wa mafuta ghafi kutoka Lokichar hadi Lamu kuanza 2020

July 17th, 2019 2 min read

NA KALUME KAZUNGU

MRADI wa ujenzi wa bomba la kusambazia mafuta ghafi kutoka Lokichar, Kaunti ya Turkana hadi kwenye eneo la Mradi wa Bandari Mpya ya Lamu (Lapsset) huko kililana utaanza mwaka 2020 badala ya tangazo la awali kwamba mradi huo ungeanza 2022.

Hii ni kufuatia mkutano wa washikadau ulioandaliwa eneo la Mokowe, Kaunti ya Lamu Jumanne na kuwaleta pamoja wahusika wanaotekeleza utafiti wa kisayansi kuhusu athari za mazingira (ESIA) kuhusu bomba hilo la mafuta na viongozi wa serikali ya kitaifa na ile ya kaunti ya Lamu.

Kwenye mkutano huo, iliafikiwa kuwa mradi huo wa bomba la mafuta ghafi utaanza mwaka ujao, ikizingatiwa kuwa ripoti ya utafiti unaoendelea wa ESIA kuhusu mradi huo huenda ikakamilika kabla ya mwisho wa mwaka huu.

Akihutubu wakati wa kikao hicho, Meneja wa Lapsset, tawi la Lamu, Salim Bunu alitaja mradi wa bomba hilo la mafuta kuwa wa natija kubwa kwa wakazi wa Lamu na pia kaunti zote sita ambapo mradi huo utapitia.

Alisema punde kazi ya ujenzi wa bomba hilo la mafuta ghafi utakapoanza mwakani, vijana wengi wa Lamu na kaunti zingine watajipatia ajira.

Kaunti sita ambazo bomba hilo la mafuta limepangwa kupitia ni Turkana, Samburu, Isiolo, Meru, Garissa na Lamu.

Bomba hilo la mafuta ghafi ambalo ni la urefu wa kilomita 820 ni mojawapo ya vipengele vinavyojumuishwa katika mradi mkuu wa Bandari ya Lamu (Lapsset).

“Tunafurahia kwamba leo tumekutanika hapa kujadiliana kuhusu suala la ujenzi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Lokichar hadi hapa Lamu. Tumejulishwa kwamba mradi huo uko kwenye hatua za mwisho mwisho kabla ya shughuli za ujenzi kuanza rasmi 2020.

“Wosia wangu kwa jamii ya Lamu ni kwamba tushikane na kuukaribisha mradi huu ambao nio mojawapo ya vigezo vya Lapsset. Ninaamini zaidi ya vijana 500 wa Lamu ambao wamehangaika muda mrefu kwa kukosa kazi watapata ajira punde mradi utakapoanza,” akasema Bw Bunu.

Mbunge wa Lamu Mashariki, Athman Sharif ambaye alikuwepo kwenye mkutano huo alisisitiza haja ya wakazi wa Lamu kupewa kipaumbele kiajira punde mradi huo wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi utakapong’oa nanga.

Bw Sharif aidha aliitaka serikali kuhakikisha malalamishi yote ambayo wananchi wa Lamu wako nayo kuhusu mradi huo yanatatuliwa kikamilifu kabla ya mradi kuanzishwa rasmi mwakani.

“Huu ni mradi wa maana sana kwa Lamu ambalo ni eneo lililoshuhudia miongo kadhaa ya utelekezaji. Cha msingi ni serikali kuhakikisha inawashirikisha vilivyo wananchi wa hapa. Pia wasikie vilio vyao na kuvitatua kikamilifu. Najua kuna wale watakaoondoshwa kwenye ardhi zao ili kupisha mradi. Lazima wananchi kama hao wafidiwe kikamilifu,” akasema Bw Sharif.

Bw Mohamed Kubwa ambaye alimwakilisha Mbunge Mwakilishi Mwanamke wa Kaunti ya Lamu, Bi Ruweida Obbo, alisisitiza haja ya serikali na mwekezajio wa mradi kuhakikisha athari zozote za kimazingira ambazo huenda zikachangiwa na mradi huo zinashughulikiwa na kutatuliwa ipasavyo.

Mradi huo uko chini ya ufadhili mkuu wa serikali ya kitaifa kwa ushirikiano na makampuni ya mafuta, ikiwemo ile ya Tullow Oil Kenya B.V, Africa Oil Turkana Ltd na Total Oil.