Makala

Mradi wa maji kusaidia kupunguza wizi wa mifugo na ujangili  


WAKAZI katika vijiji vya Chesogon na Empowol, mpakani mwa Kaunti ya Pokot Magharibi na Elgeyo Marakwet, wamepata afueni baada ya mradi wa usambazaji maji kuzinduliwa.

Mradi huo wa mamilioni ya pesa unatekelezwa na halmashauri ya North Rift Water Works Development Agency (NRVWWDA), na unatarajiwa kusaidia kudumisha amani na kupunguza mizozo kati ya jamii hasimu zinazoishi eneo hilo, Bonde la Kerio.

Eneo hilo likiwa kame, wanatarajia kupata maji safi.

Kwa muda mrefu, eneo hilo limekosa vituo vya maji suala ambalo hupelekea jamii za wafugaji wa kuhamahama kutoka eneo moja hadi lingine kusaka maji na nyasi.

Ukitarajiwa kuleta mabadiliko, utahudumia jamiii ambazo kwa historia zimekuwa zikizozana  kuhusu maji na malisho ya mifugo – nyasi.

Ulianzishwa Machi mwaka huu, 2024.

“Hatuna nguvu ya kuendea maji mbali. Tunashukuru kwa mradi huu. Tunahitaji maendeleo,” alisema James Lokadio mkazi wa Chesegon.

Mwenyeji huyo, alisema kwa sababu ya kukosa maji na nyasi za mifugo, jamii zimekuwa zikizozana kwa muda.

Paul Chonguria, mkazi mwingine, aliambia Taifa Dijitali kwamba wana mifugo wengi ni kuzinduliwa kwa mradi huo ni afueni.

Hata hivyo, alihimiza serikali za kaunti husika kuchimba vidimbwi vingi ili kufanikisha ufugaji na kilimo.

“Mradi huu wa maji umeleta utulivu katika eneo hili ambalo lilikuwa na mizozo mingi ya kudumu,” alisema.

Aidha, wamekuwa wakitembea zaidi ya kilomita kumi kutafuta maji.

Mahangaiko sasa yapungua

“Tumekuwa tukitafutia mifugo wetu maji masafa marefu, na inachosha. Tunashukuru mahangaiko hayo sasa yamepungua,” alisema mwenyeji Alice Cheruiyot.

Aliyekuwa Gavana wa Pokot Magharibi Prof Lonyangapuo ambaye sasa ni mwenyekiti wa Halmashauri ya Maji eneo la Kaskazini mwa Bonde la Ufa, pamoja na afisa mkuu wa asasi hiyo, Edwin Cheruyoit walisema kuwa mradi huo utasaidia wafugaji kukaa mahali pamoja na kuhusika kwenye miradi za maendeleo.

Isitoshe, viongozi hao walielezea imani yao kuwa mradi huo wa maji utasaidia kudhibiti visa vya wizi wa mifugo na uhalifu.

“Maji ni adimu katika eneo hili. Kuna changamoto ya nyasi na mradi huu utapunguza mizozo kati ya jamii za  Marakwet na Pokot. Wakazi hupigana kwa sababu ya maji na nyasi,” alisema Prof Lonyangapuo.

Alisema kuwa mradi huo unatarajiwa kunufaisha zaidi ya familia 4,000 na mifugo 15,000

“Hatua hii itaisaidiia na kulinda watu wetu kuwacha kuhamahama hadi nchini zingine kusaka maji,” alisema Gavana huyo wa zamani.

Huku uzinduzi wa mradi huo wa maji safi ukipaniwa kuangazia kero ya magonjwa yanayosababishwa na uchafu na zaidi ya yote kukabiliana na umaskini, jamii za Pokot na Marakwet zinatarajiwa kushirikiana katika kuuongoza.

“Nguzo kuu ya afya bora ni kuwepo kwa maji safi. Gapu hii itaangaziwa,” Mbunge wa Sigor Peter Lochakapong alisema.

Viongozi hao wa kisiasa, walielezea imani yao kwamba miradi ya aina hiyo ikizinduliwa kwa wingi Bonde la Kerio visa vya wizi wa mifugo na ujangili vinavyoshuhudiwa mara kwa mara vitaangaziwa pakubwa.

[email protected]