Makala

Mradi wa NiE ni lulu inayowaniwa Shuleni Sangenyi, Taita Taveta

February 25th, 2020 2 min read

NA CHRIS ADUNGO

SHULE ya Msingi ya Sangenyi katika Kaunti ya Taita- Taveta ni miongoni mwa shule nyingi za humu nchini ambazo kwa sasa zinatambua umuhimu wa mradi wa Newspapers in Education (NiE) unaoendeshwa na kampuni ya Nation Media Group (NMG).

Kupitia mradi huu, NMG inayatumia gazeti lake la Taifa Leo kuimarisha viwango vya kusomwa na kufundishwa kwa Kiswahili na masomo mengine katika shule za msingi na za upili.

Bi Agnes Kililo ambaye ni mwalimu wa Kiswahili katika Shule ya Msingi ya Sangenyi, anakiri kwamba matokeo bora yanayojivuniwa na wanafunzi wake katika mitihani ya kitaifa ya KCPE ni zao la NiE, mradi ambao kwa mtazamo wake unazidi kubadilisha pakubwa sura ya usomaji na ufundishaji wa Kiswahili shuleni humo.

Kwa mujibu wa mwalimu huyo, wengi wa wanafunzi wake wanaothamini na kuchangamkia usomaji wa Taifa Leo na kushiriki Shindano la Uandishi wa Insha katika gazeti hili hudumisha umahiri wao katika lugha kwa kukwangura alama za juu zaidi katika mithani ya Kiswahili.

Walimu na wanafunzi wa Shule ya Msingi ya Sangenyi wanasifia pia majaribio ya mitihani ambayo huchapishwa katika gazeti hili la Taifa Leo kati ya miezi Februari na Novemba kuwa mhimili mkubwa unaozidi kuchangia matokeo bora ya wanafunzi wao katika mitihani ya kitaifa ya KCPE.

Shule hiyo ni miongoni mwa zile ambazo zimekuwa zikijinunulia nakala za gazeti la Taifa Leo na Taifa Jumapili kupitia mradi wa NiE.

Bw Maddleton Maseghe ambaye pia ni mwalimu shuleni humo, anasema kwamba majaribio hayo ya mitihani ni daraja halisi la mafanikio kwa wengi wa wanafunzi wake ambao wamechochewa kutia fora katika Kiswahili huku wakihimizwa kuyathamini masomo mengine kwa kiwango sawa.

Mwalimu huyo anazisihi shule nyinginezo za humu nchini kuiga mfano wao ili kuimarisha viwango vya kujiandaa kwa wanafunzi kwa mitihani ya kitaifa ya KCPE.

“Majaribio hayo huwaondolea hofu wanafunzi wengi wanaotazamia kutahiniwa kwa kuwa huwapa hali ya kujiamani. Hili huwatia motisha ya kujituma maradufu kila wanapotumia maswali na majibu ya mitihani gazetini kujitia kwenye mizani na kujikosoa wakati mwingine bila ya hata msaada wa walimu wao,” anasema Bw Maseghe katika kauli inayoungwa mkono na Bi Mercy Mwashighadi, Bw Michael Njulu na Bi Dorothy Mwanyasi ambao kwa pamoja, wamepania kuhakikisha kwamba gurudumu la Kiswahili halikwami kabisa katika Shule ya Msingi ya Sangenyi.

Bw Walter Ziri ambaye ni Mwalimu Mkuu shuleni Sangenyi anahisi kwamba tayari matunda ya uwapo wa Chama cha Kiswahili shuleni humo tayari yameanza kuvunwa.

hasa ikizingatiwa ukubwa wa kiwango cha jinsi wanafunzi wanavyolichapukia somo la Kiswahili pamoja na jinsi wanavyotumia lugha hiyo kwa usanifu zaidi katika mawasiliano.

Isitoshe, anaungama kuwa baadhi ya mafanikio ya hadi sasa yanayojivuniwa na chama ni ari ya Sangenyi katika kuibua mabingwa wengi katika Shindano la Uandishi wa Insha linaloendeshwa na gazeti hili la Taifa Leo.