Makala

Mradi wa Ushanga Initiative wawawezesha wanawake kutengeneza bidhaa za kimataifa

February 19th, 2020 1 min read

Na MAGDALENE WANJA

MRADI wa Ushanga Initiative ulianzishwa mnamo mwaka 2017 kama njia mojawapo ya kuwawezesha wAnawake kutoka kwa jamii za wafugaji kujitegemea.

Kwa muda mrefu wanawake kutoka katika jamii hizo hawakuwa na haki ya kumiliki mali yoyote ila tu mapambo waliotengeneza kwa kutumia shanga.

Mapambo hayo hayakuwa na manufaa yoyote ya kiuchumi kwao.

Lengo kuu la serikali lilikuwa ni kuwapa nafasi za kazi ili kuwapa mapato kutokana na ujuzi wao.

Afisa mkuu mtendaji wa Ushanga Initiative Kenya Bi Dorothy Mashipei aonyesha baadhi ya bidhaa zilizotengenezwa kwa shanga. Picha/ Magdalene Wanja

Baadhi ya bidhaa ambazo wamekuwa wakizitengeneza zimevutia ulimwengu hasa katika ulimwengu wa muziki ambapo wasanii wanapenda kuzitumia.

Video ya muziki ya wasanii Yemi Alade akimshirikisha mshindi wa tuzo ya Grammy Angelique Kidjo imewavutia watu wengi na imeweza kutazamwa mara zaidi ya milioni mbili chini ya muda wa majuma mawili.

Wimbo huo kwa jina ‘Shekere’ uko katika albamu yake kwa jina “Woman of Steel” na video hiyo ilirekodiwa katika mbuga ya wanyama ya Maasai Mara.

Afisa mkuu mtendaji wa Ushanga Initiative Kenya Bi Dorothy Mashipei aonyesha baadhi ya bidhaa zilizotengenezwa kwa shanga. Picha/ Magdalene Wanja

Matumizi ya rangi tofauti katika video hiyo yanaashiria jinsi utamaduni wa jamii za Kenya na hasa wa Kimaasai umekita mizizi.

Kulingana na afisa mkuu mtendaji wa Ushanga Initiative Kenya Bi Dorothy Mashipei ni kwamba kupitia mradi huo, wanawake wameelimishwa jinsi ya kutengeneza bidhaa ambazo zinaweza kuuzwa katika soko la kimataifa.

“Wanawake katika jamii hizi wameweza kuondoa dhana ya kuhurumiwa na wameweza kumiliki mali zaidi kupitia biashara hiyo,” asema Bi Mashipei.

Anaongeza kuwa ujuzi huo pia wameutumia kuunda bidhaa za kisasa na kuwawezwsha kufanya vyema zaidi katika soko za kimataifa.