Mrembo aliyeegesha gari katikati ya barabara kupokea busu atozwa faini ya Sh20,000

Mrembo aliyeegesha gari katikati ya barabara kupokea busu atozwa faini ya Sh20,000

NA RICHARD MUNGUTI

KIDOSHO mwenye umri wa miaka 26 aliyesimamisha gari katikati ya barabara kupokea busu la mpenziwe atatoboka faini ya Sh20,000 ama atumikie kifungo cha miezi sita.

Kisa hiki kilichotokea katika barabara kuu ya Thika-Nairobi kilisababisha msongamano mkubwa wa magari.

Wenye magari walipiga honi huku wengine wakiwafokea wapenzi hao.

Polisi waliposongea karibu na gari alimokuwa Tabby Ndung’u hawakufurahia kwa ‘kumkatizia raha’ mwanadada huyo.

Kwa hasira, Tabby alichomoka kutoka kwa gari hilo na kuwafokea maafisa wawili wa polisi wanaume wanaoshika doria katika barabara hiyo yenye shughuli nyingi.

 “Mshtakiwa alichomoka ndani ya gari na kwa hasira aliwafokea maafisa wawili wa polisi kwa matusi,” kiongozi wa mashtaka alimweleza hakimu Kyambia.

Hatuwezi kuchapisha matusi Tabby aliwatukana maafisa hao wa usalama.

Kwa vile maafisa wa kiume wa polisi hawawezi kumkamata mwanamke, walipiga ova ova katika kituo cha polisi cha Kasarani na kuitisha msaada wa polisi wa kike.

“Polisi wanawake walifika mahala hapo karibu na Thika Road Mall (TRM) na kumtia mbaroni Tabby,” mahakama ilifahamishwa.

Mshtakiwa alikiri shtaka la kuzua vurugu na kuhatarisha amani Januari 24, 2023 karibu na TRM.

Wakati wa majibizano hayo makali, Tabby aliwataka Polisi wamfyatulie risasi.

Katika kituo cha polisi cha Kasarani Tabby alishtakiwa kwa kuzua vurugu kwa lengo la kuhatarisha amani kinyume cha Kifungu 95 (1)(b) cha sheria za uhalifu na kushiriki ‘tabia mbaya’ hadharani kinyume cha sheria nambari 94(1) za uhalifu.

Hakimu alielezwa wakati Tabby na mpenziwe walikuwa wanabusiana msongamano wa magari ulikumba barabara hiyo.

Polisi waliwafumania wapenzi hao wakibusiana kwa shauku na hamu kuu katikati ya barabara.

Lakini alipokatizwa raha, Tabby aliwafokea polisi hao kutoka kitengo cha kutunza barabara kuu cha Critical Infrastructure Protection Unit (CIPCU).

Kwa kila shtaka Bw Kyambia alimtoza mshtakiwa faini ya Sh10,000 ama atumikie kifungo cha miezi sita gerezani.

  • Tags

You can share this post!

NGUVU ZA HOJA: Walimu wa lugha ya Kiswahili waandaliwe...

Tottenham wasuka upya safu yao ya mbele kwa kusajili fowadi...

T L