Habari Mseto

Mrengo wa Ruto wataka Raila aandikishe taarifa kuhusu sakata ya dhahabu bandia

May 25th, 2019 1 min read

Na CHARLES WASONGA na DPPS

BAADHI ya wabunge wa Jubilee kutoka Narok wamemtaka Mkurugenzi wa Upelelezi wa Jinai (DCI) George Kinoti kumlazimisha kiongozi wa ODM Raila Odinga kuandikisha taarifa kuelezea kile anachofahamu kuhusu sakata ya dhahabu bandia.

Lakini akiongea dakika chache baadaye katika eneobunge la Shinyalu, Kaunti ya Kakamega Bw Odinga alikariri kwamba ni yeye alifichua sakata hiyo na kuwataka Wakenya kuruhusu uchunguzi uendelee ili wahusika wakamatwe.

Wakiongea jana katika eneo la Suswa, Kaunti ya Narok walipoandamana na Naibu Rais William Ruto katika ziara ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo, wabunge watano walisema Bw Odinga ni mhusika mkuu katika ulaghai huo wala si mfichuzi alivyodai juzi akiwa Kisii.

Uchunguzi

“Tunahimiza DCI kuendelea na kazi yake ya uchunguzi kuhusu sakata ya dhahabu bandia. Lakini sharti Bw Kinoti (George) amwite Raila aelezee kile anachofahamu kuhusu sakata hii kwa sababu sasa ni wazi kuwa yeye ni sehemu ya wahalifu walioshiriki ulaghai huo,” akasema Mbunge Mwakilishi wa Wanawake Narok katika Bunge la Kitaifa Bi Soipan Tuya.

Naye Mbunge Maalumu Bw David Sankok alipuuzilia mbali madai ya Odinga kwamba yeye ndiye alifichua sakata hiyo kwa maafisa wa usalama akisema kiongozi huyo wa ODM ni mmoja waliofaidi kutokana na sakata hiyo.

“Mbona anadanganya Wakenya kwamba alienda Dubai kujadiliana na Mfalme ilhali ukweli ni kuwa alienda kupokea pesa,” akadai Bw Sankok.

Wengine waliomshambulia Bw Odinga kuhusiana na sakata hiyo, ambapo inadaiwa familia ya Mfalme wa Dubai ilipoteza Sh400 milioni, walikuwa ni Gavana wa Narok Samuel Tunai, Mbunge wa Narok Mashariki Ken Aramat na mwenzake wa Mwala Vincent Musyoka.