Habari Mseto

Mrithi wa Sonko jijini aanza kusakwa

December 20th, 2020 2 min read

Na COLLINS OMULO

SIKU chache baada ya aliyekuwa Gavana wa Nairobi, Bw Mike Sonko kufurushwa mamlakani na Seneti, harakati za kisiasa zimeanza kuhusu ni nani atakayechukua wadhifa huo.

Harakati hizo zinasukumwa na siasa za handisheki kati ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga, mirengo ya ‘Kieleweke’ na ‘Tangatanga’.

Tayari, watu kadhaa wamejitokeza kujaribu bahati yao kutwaa nafasi hiyo, kwenye uchaguzi mdogo unaotarajiwa kufanyika mwaka 2021.

Miongoni mwa wale wanaotajwa ni mwanasiasa Peter Kenneth, ambaye aliwania urais mnamo 2013, aliyekuwa mbunge wa Dagoretti Kusini Dennis Waweru na Askofu Margaret Wanjiru, aliyehudumu kama mbunge wa Starehe.

Wengine wanaotajwa ni mfanyabiashara Agnes Kagure, aliyekuwa Katibu wa Baraza la Jiji la Nairobi Philip Kisia na aliyekuwa Gavana wa Kiambu, Bw William Kabogo.

Ikizingatiwa Kaunti ya Nairobi ina idadi kubwa ya watu, mielekeo ya kikabila, ushindani wa vyama na uwepo wa vijana ni miongoni mwa masuala makuu yanayotarajiwa kujitokeza kwenye kinyang’anyiro hicho.

Wengine ni pamoja na mfanyabiashara Agnes Kagure, aliyekuwa Katibu wa Baraza la Jiji la Nairobi Philip Kisia na aliyekuwa gavana wa Kiambu, Bw William Kabogo.

Ikizingatiwa Kaunti ya Nairobi ina idadi kubwa ya watu; mirengo ya kikabila, ushindani wa vyama na mchango wa vijana ni miongoni mwa masuala makuu yanayotarajiwa kushamiri kinyang’anyiro hicho.

Uchaguzi huo pia utakuwa muhimu sana kwani unatazamiwa kutoa taswira ya mwelekeo wa kisiasa nchini huku uchaguzi mkuu wa 2022 ukikaribia.

Spika wa Bunge la Kaunti ya Nairobi, Bw Benson Mutura, anatarajiwa kuhudumu kwa siku 60 kama Kaimu Gavana kabla ya uchaguzi huo mdogo kufanyika.

Duru ziliambia Taifa Leo kwamba, ikizingatiwa nafasi hiyo ilishikiliwa na chama cha Jubilee (JP), kinapanga kumsimamisha mgombea mwingine.

Chama cha ODM kimeombwa kumuunga mkono mgombea huyo, huku kikiahidiwa nafasi ya mgombea-mwenza.

Inaelezwa kwamba hatua hiyo inalenga kudumisha muafaka wa handisheki.

Jubilee iliwaunga mkono wagombea wa ODM kwenye chaguzi ndogo za maeneobunge ya Kibra na Msambweni.

“Kuna uwezekano mkubwa nafasi hiyo ikatwaliwa tena na Jubilee kupitia uungwaji mkono wa ODM. Hili linatokana na chaguzi za awali ambapo vyama hivyo viwili vimeungana kumpigia debe mwaniaji mmoja. Bw Sonko alikuwa amechaguliwa kwa tiketi ya Jubilee, hivyo ni vyema chama kurejeshewa nafasi hiyo huku naibu akitoka katika ODM,” zilieleza duru hizo.

Hatua hiyo si nadra kwani mpangilio kama huo ulizingatiwa kwenye uchaguzi wa Spika.

Katika shughuli hiyo mnamo Agosti, Bw Mutura wa Jubilee aliungwa mkono na ODM, huku chama hicho cha chungwa kikipewa nafasi ya Naibu Spika iliyomuendea Diwani Geoffrey Majiwa wa wadi ya Babadogo.

Kwa upande mwingine, mrengo wa ‘Tangatanga’, unaoongozwa na Naibu Rais William Ruto, unatarajiwa kumsimamisha mgombea wake kwenye uchaguzi huo mdogo wa kumrithi Bw Sonko.

Mrengo huo uliwasimamisha wagombea wake katika chaguzi ndogo za maeneobunge ya Kibra na Msambweni.

Huko Kibra, Kaunti ya Nairobi, ‘Tangatanga’ walimpigia debe mwanasoka Macdonald Mariga akikabana na Bw Imran Okoth, aliyewania kwa tiketi ya chama cha ODM.

Hii ni licha ya Rais Kenyatta kutangaza kuwa angemuunga mkono Bw Okoth – mshindi wa uchaguzi huo.

Katika eneo la Msambweni, Kaunti ya Kwale, Dkt Ruto na washirika wake walimuunga mkono mwaniaji huru Feisal Bader – ambaye ndiye aliibuka mshindi.

Bader alipata kura 15, 251 akimlaza Bw Omar Boga wa ODM aliyezoa kura 10,444.

Inadaiwa kuwa, tayari mrengo huo wa ‘Tangatanga’ umemwidhinisha Bi Wanjiru kama mgombeaji wake katika uchaguzi mdogo wa ugavana Nairobi.