Habari Mseto

Msaada wa MCA wa ‘ambulensi’ ya probox wafaidi wakazi

April 10th, 2024 2 min read

Na VITALIS KIMUTAI

NI kawaida kuona gari aina ya Toyota Probox katika barabara za Kenya na linajulikana kwa matumizi mengi.

Gari hilo dogo hutumika kwa shughuli mbalimbali za kila siku, kuanzia kubeba abiria hadi kusafirisha bidhaa na imekuwa sehemu muhimu ya maisha ya kila siku kwa Wakenya wengi katika maeneo ya mashambani na mijini.

Hata hivyo, katika wadi ya Chemaner, Kaunti ya Bomet, Probox imebadilika na kuwa ishara ya matumaini katika sekta ya afya.

Huku akikabiliwa na hali halisi ya upatikanaji wa huduma za afya katika wadi yake ambapo wagonjwa mara nyingi wanatatizika kufika kwenye vituo vya matibabu kutokana na hali mbaya ya barabara, diwani wa Chemaner Richard Ruto Kigaru alivalia njuga mwenyewe suala hilo.

Alinunua gari aina ya Toyota Probox na kulikabidhi kituo cha afya cha Chemaner, sio kama gari la kawaida kwa matumizi ya kila siku, bali kama “ambulensi”.

Ulikuwa mchango wa kibinafsi unaolenga kuimarisha huduma za dharura za matibabu lakini sasa umezua maoni tofauti miongoni mwa wakazi na hata washikadau.

“Niliponunua Toyota Probox na kukabidhi kituo cha afya, sikutarajia ingeweza kuzua maoni mseto. Ningependa kufafanua kuwa gari hilo ni la uokoaji wala si “ambulensi” inavyodaiwa,” Bw Kigaru alisema.

Aliendelea: “Ukweli wa hali halisi ni kwamba kutokana na hali ya barabara kuwa mbovu, wananchi wanashindwa kufika kwenye vituo vya afya huku akina mama wajawazito wakijifungulia kando ya barabara wakipelekwa hospitalini.

Viti vya nyuma vya gari viliondolewa na nafasi ilirekebishwa ili kumweka mgonjwa, dereva na abiria wa ziada wakikaa viti vya mbele.

Huku baadhi ya wakazi wakipongeza mpango wa MCA, kama juhudi yenye nia njema kushughulikia mahitaji ya dharura ya sekta ya afya, wengine wanasema sio suluhu kwa tatizo kubwa.

Kitendo kisicho cha kawaida cha Bw Kigaru kimezua mjadala mkali ndani ya jamii ya eneo hilo, na kuzua maswali kuhusu utoshelevu wa rasilimali za afya na wajibu wa viongozi kwa raia.

Bi Mary Koech, mkazi wa kijiji cha Chambori alisema watoto, wazee na akina mama wajawazito wamekumbwa na mateso mengi wakitafuta matibabu.

“Ni faraja kwa wakazi wa kata ya Chemaner ambao baadhi yao wamepoteza maisha kutokana na magonjwa na majeraha kwa kushindwa kufikishwa hospitalini kwa wakati unaofaa,” alisema.