Habari Mseto

Msaada wa Sonko kwa wanaotafunwa na njaa Turkana

March 20th, 2019 1 min read

Na PETER MBURU

WAKATI viongozi wa serikali kuu za zingine za kaunti wakizidi kujitia hamnazo kuhusu hali ya kiangazi na njaa inayokumba wakazi wa Turkana, Baringo na maeneo mengine ya nchi, Magavana wa Nairobi Mike Sonko na John Lonyangapuo wamekiri kuwa hali ni mbaya na kuanza kutoa misaada.

Viongozi hao Jumatano walijitolea kuwaokoa wakazi wanaoteseka, baada ya kutoa chakula cha msaada pamoja na maji kuwaokoa maelfu ya Wakenya ambao wamekuwa wakiteseka.

Gavana Sonko Jumatano alitoa mizigo ya unga, mafuta na vyakula vingine ambavyo vilipakiwa kwenye magari kusafirishwa hadi kaunti ya Turkana kuwasaidia watu, wakati akiwataka viongozi wengine kuchukua hatua kama yake, badala ya kupiga siasa tu.

Hatua ya gavana huyo ilifurahiwa na Wakenya wengi ambao wamempongeza kwa moyo wake wa ukarimu na ishara ya uongozi wa busara.

“Kama balozi wa matendo mema, timu yangu inapakia vyakula na vitu vingine ambavyo vitasambazwa Kaunti ya Turkana kuwaokoa Wakenya ambao wanateseka na njaa. Nawaomba viongozi wengine pia kufanya kitu kumaliza janga hili,” akasema Bw Sonko.

Prof Lonyangapuo naye alikiri kuwa watu wawili wameaga dunia katika kaunti yake, kinyume na madai ya serikali kuu kuwa hakuna mtu ambaye amefariki, akisema tayari ameanza kuwapa wakazi maji.

“Hata kuna watu wawili wamethibitishwa kufa kwenye mpaka wa kaunti yangu, Baringo na Turkana Kusini. Hata maji hakuna, tumeanza kusambaza kila shule ama mahali kuna tenki za kuyahifadhi iliwapate maji,” akasema gavana huyo.

Prof Lonyangapuo alisema kiwango cha chakula ambacho serikali ya kaunti yake iko nacho ni kidogo na hivyo wanahitaji mkono wa ziada kutoka kwa serikali kuu.