Habari MsetoSiasa

Msafara wa Naibu wa Joho washambuliwa kupinga vioski kubomolewa

February 21st, 2018 2 min read

Baadhi ya magari ya kaunti ya Mombasa yaliyopigwa mawe na vijana kutoka eneo la Senti Kumi, Likoni Februari 20, 2018. Picha/ Wachira Mwangi

Na HAMISI NGOWA na MOHAMED AHMED

MAGARI saba likiwemo la Naibu Gavana wa Kaunti ya Mombasa William Kingi, yaliharibiwa vioo baada ya kushambuliwa kwa mawe na vijana katika eneo bunge la Likoni Jumanne, wakihofia kuwa vibanda vyao kando ya barabara vitabomolewa.

Dkt Kingi alikuwa ameandamana na mbunge wa eneo hilo, Bi Mishi Mboko pamoja na madiwani wakati msafara wake uliposhambuliwa na kundi la vijana zaidi ya 30.

Alikuwa katika barabara ya Senti Kumi kujionea sehemu ambayo serikali ya Kaunti inapanga kuweka kituo cha magari ili kupunguza msongamano katika steji iliyopo kwa Kivuko cha Likoni wakati kundi la vijana lilipowashambulia.

Akizungumza na Taifa Leo, Dkt Kingi alisema ziara yake eneo hilo ilijiri siku moja baada ya wawakilishi wa wadi katika eneo hilo kuitaka ofisi ya gavana kuzuru eneo hilo kwa lengo la kujionea miradi inayosubiri kukamilishwa.

“Nilikuwa katika ziara ya kujifahamisha ni miradi gani inayohitaji kukamilishwa na ile ambayo wakazi wanataka serikali ya Kaunti iweze kuwajengea, lakini kwa bahati mbaya vijana wakatushambulia,’’ akasema.

Alisema serikali ya Kaunti haitasita kuchukua sheria dhidi ya mijengo iliyojengwa kwenye sehemu zisizohitajika kuwa na majengo.

Gari hili aina ya Ford, ni baadhi ya magari ya kaunti ya Mombasa yaliyopigwa mawe na vijana kutoka eneo la Senti Kumi, Likoni, Mombasa Februari 20, 2018. Picha/ Wachira Mwangi

Bi Mboko alisema vijana hao ndio hujihusisha na visa vya unyakuzi wa ardhi za umma akisema serikali kuu na ile ya Kaunti kamwe hazitakubali maovu hayo kuendelea.

Alisema vijana hao wanatumiwa na baadhi ya matapeli wa ardhi ambao nia yao ni kujinufaisha kupitia ulaghai wa ardhi za umma.Alisema inasikitisha kwamba vijana hao sasa wameanza kunyemelea hata ardhi za shule na zile za barabara baada ya kumaliza kuuza shamba la Waitiki.

“Hatuwezi kukubali hali kama hii kuendelea ambapo ardhi hata zile zilizotengwa kwa ujenzi wa shule za umma zinanyakuliwa,” akasisitiza.

Inadaiwa vijana hao walishambulia msafara huo baada ya kudhani kuwa vibanda vilivyojengwa karibu na barabara vitabomolewa.
OCPD wa Likoni, Bw Benjamin Rotich alisema waliohusika ni “wahuni na watachukuliwa hatua.”

“Tumetuma kundi letu kuwafuata watu hao. Ikiwa wako sehemu hiyo kinyume cha sheria lazima waondolewe. Kwani wao ni kina nani kuchukua sheria mikononi mwao?” aliuliza Bw Rotich.

Hali hiyo ilimfanya Dkt Kingi na msafara wake kukatiza safari yao.