Habari za Kaunti

Msafara wa Rais Ruto waacha wabunge walioandamana naye kwa mataa Nyahururu

Na WAIKWA MAINA June 23rd, 2024 1 min read

WABUNGE walioandamana na Rais William Ruto katika hafla ya kanisa la ACK, Nyahururu waliona siku ndefu wakati msafara wa Rais ulipoondoka na kuwaacha kupambana na Gen Z.

Kiongozi wa nchi alikuwa anahudhuria kutawazwa kwa Kasisi Samson Mburu kuwa Mkuu wa ACK Nyahururu, na kama ilivyo kawaida, wabunge wa Kenya Kwanza na viongozi wengine waliandamana naye.

Lakini ulipofika wakati wa kuondoka, vijana wanaopinga Mswada wa Fedha 2024 walisubiri msafara wa Rais katika lango la watu mashuhuri la Shule ya Msingi ya Ndururi wakiimba nyimbo za kumkashifu.

Hata hivyo, maafisa wa ulinzi walifaulu kumkingia Rais akaondoka, na kuacha wabunge wamekwama.

Iliwalazimu wanasiasa hao kutafuta mbinu za kujinusuru huku umati wa vijana waliokuwa na ghadhabu ukiendelea kuongezeka.