Habari Mseto

Msagaji asakwa kwa kuchoma nyumba 40 kwenye mzozo wa ushoga

July 3rd, 2019 1 min read

Na BENSON MATHEKA

POLISI jijini Nairobi, wanamsaka mwanamke anayeshukiwa kuwasha moto ulioteketeza zaidi ya nyumba 40 mtaani Kibra katika mzozo wa mapenzi uliohusu wanawake watatu wasagaji.

Inasemekana kuwa mwanamke huyo alikasirika baada ya kumpata mwanadada mpenzi wake akiwa na mwanamke mwingine Jumapili usiku.

Kulingana na wakazi na maafisa wa polisi, mshukiwa alizua kisanga na kumjeruhi vibaya mmoja wa wanawake hao akidai alikuwa amemsaliti.

Wakazi walisema kwamba mshukiwa alikasirika mpenzi wake alipomsaliti kwa kuanza uhusiano wa kimapenzi na mwanamke mwingine.

“Mwanamke aliyejeruhiwa alikimbizwa hospitali na mpenzi wake mpya. Kilikuwa kisanga cha kuaibisha. Sijawahi kuona wanawake wasagaji wakipigania mpenzi mmoja,” alisema mkazi aliyejitambulisha kama Osman Ishmail.

Alisema mshukiwa anayeaminika kuwa raia wa kigeni, alichoma nyumba na moto ukasambaa haraka katika mtaa huo wa mabanda na kusababisha hasara kubwa.

“Zaidi ya nyumba 40 ziliteketea na kuacha watu zaidi ya 100 bila makao,” alisema.

Chifu wa eneo la Makina, Bw Hillary Chumo alisema watu walilazimika kukesha kwenye baridi baada ya mali yao kuteketea.

Mwanamke huyo alitoroka baada ya kuwasha moto huo. Kisa hicho kilitokea karibu na Mahakama ya Kibera na nyuma ya msikiti unaendelea kujengwa eneo hilo.

Bw Chumo alisema kwamba wazima moto walikuwa na wakati mgumu kufika eneo la mkasa kwa sababu hakuna barabara.

Kulingana na wakazi, mshukiwa alikuwa ameonya mpenzi wake kwamba angemfanya ajute kwa kumsaliti alipogundua alikuwa amepata mpenzi mwingine.

: Mapenzi baina ya watu wa jinsia moja ni haramu Kenya na wanaopatikana na hatia wanaweza kufungwa jela miaka 14. Hivi majuzi, mahakama iliamua kwamba katiba ya Kenya hairuhusu vitendo vya ushoga na usagaji katika kesi iliyowasilishwa na wanaharakati wakitaka vitendo vyao vihalalishwe.

Katika nchi 71 kote ulimwenguni vitendo vya mapenzi baina ya watu wa jinsia moja ni haramu.

Barani Afrika, ni Afrika Kusini na Botswana ambazo ziliharamisha ushoga na usagaji hivi majuzi.