Msajili ajitenga na kashfa ya usajili vyamani

Msajili ajitenga na kashfa ya usajili vyamani

Na WANDERI KAMAU

MSAJILI wa Mkuu wa Vyama vya Kisiasa nchini, Bi Anne Nderitu, amesema afisi yake haipaswi kulaumiwa kwa kashfa ambapo maelfu ya Wakenya walijipata wakiwa wameorodheshwa kama wanachama wa vyama tofauti vya kisiasa.

Badala yake, msajili huyo alisema hali hiyo inalingana na maelezo ambayo Wakenya walitoa kwa vyama vya kisiasa walipokuwa wakijisajili kama wanachama.

Kwenye mahojiano Jumapili, Bi Nderitu aliwashauri Wakenya waliojipata katika hali hiyo kuviandikia barua vyama husika kupitia kwa afisi yake ili kubadili hali ya uanachama wao.

“Afisi yangu haipaswi kulaumiwa hata kidogo kwani maelezo tuliyo nayo huwa tunayapata kutoka vyama vya kisiasa. Kazi yetu huwa ni kuyaweka kwenye sajili yetu kama tunavyohitajika kisheria. Hivyo, wale ambao wamejipata wameorodheshwa kama wanachama wa vyama tofauti vya kisiasa wanapaswa kuvilaumu,” akasema.

Kauli yake inafuatia hali ambapo maelfu ya Wakenya walijipata wamesajiliwa kama wanachama wa vyama tofauti katika hali ya kutatanisha wiki iliyopita.Baadhi walilalamika hawajawahi kujisajilisha kama wanachama wa chama chochote cha kisiasa.

Wengine walitaja hali hiyo kama njama ya afisi yake kutoa maelezo yao kwa vyama bila kibali chao, wakikosoa hilo kama ukiukaji wa haki zao.

Wanasheria wamesema kuwa badala ya kujitetea, afisi hiyo inapaswa kueleza wazi kilichofanyika, kwani hilo linawapa Wakenya nafasi kuishtaki mahakamani kwa kuingilia maelezo yao bila kibali chao.

“Ikiwa afisi haitatoa maelezo ya kuridhisha, basi Wakenya walioathiriwa wana haki ya kwenda mahakamani kuishtaki. Lazima pawe na ufafanuzi wa kutosha,” akasema wakili Lempaa Suyianka.

Hata hivyo, Bi Nderitu alitaja zoezi hilo kama “jaribio la kudhihirisha umahsusi wa sajili yao.”

“Badala ya lawama, hali hii imedhihirisha wazi kuwa sajili yetu ni thabiti kwani Wakenya wanaweza kuthibitisha vyama vya kisiasa ambavyo ni wanachama. Jukumu ni lao kurekebisha makosa waliyopata,”akasema.

Jana, shirika la Amnesty International lilimtaka Kamishna wa Data nchini, Bi Immaculate Kassait, kuanzisha uchunguzi kuhusu sakata hiyo.Kwenye taarifa, shirika lilisema kuwa ni ukiukaji wa sheria kwa taasisi yoyote ya serikali kutumia maelezo ya kibinafsi ya wananchi bila kibali chao.

You can share this post!

Chama chake Abbiy kifua mbele uchaguzini Ethiopia

NWRL: Umul Qura yapania kucheza kila mechi kama fainali