Michezo

Msakataji stadi wa Starlets Esse Akida sasa ni mali ya Besiktas

February 17th, 2020 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

MSHAMBULIAJI Esse Mbeyu Akida amejiunga na malkia wa soka nchini Uturuki, Besiktas yenye makao yake jijini Istanbul.

Mchezaji huyu wa zamani wa klabu za Spedag na Thika Queens ametua Besiktas akitokea FC Ramat HaSharon inayoshiriki Ligi Kuu ya Israel.

Akida, 27, alianzia soka yake katika klabu ya Moving The Goalposts (MTG) kabla ya kuchezea Spedag na kisha Thika Queens kabla ya kunyakuliwa na HaSharon mwaka 2018 kwa kandarasi ya miaka miwili.

“Nafurahia kutangaza rasmi kuwa nimejiunga na familia ya Besiktas; klabu kubwa yenye azma kubwa. Nataka kushukuru Ramat HaSharon kwa kunipatia fursa ya kwanza kabisa kucheza soka ya malipo nje ya Kenya na ninaitakia kila la kheri katika msimu mpya,” Akida amesema kwenye mtandao wake wa Twitter, Jumatatu.

Akida alianza kupata umaarufu kimataifa mwaka 2016 alipoibuka mchezaji bora (MVP) katika soka ya COTIF mjini Valencia nchini Uhispania akichezea timu ya taifa ya Kenya almaarufu Harambee Starlets.

Alishiriki katika Kombe la Afrika (AWCON) 2016 baadaye mwaka huo ambapo Kenya ilikuwa ikijitosa katika mashindano hayo kwa mara yake ya kwanza.

Akida alifunga bao lililoweka Kenya 1-0 juu dhidi ya Ghana katika mechi ya ufunguzi ya Kundi B nchini Cameroon, lakini timu yake ikaishia kupoteza 3-1 na pia kulemewa na Mali 3-1 na Nigeria 4-0 ikivuta mkia katika mashindano hayo ya mataifa manane.

Mara ya mwisho Akida alichezea Starlets ilikuwa mwaka 2018 katika mashindano ya Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) jijini Kigali nchini Rwanda.

Kenya sasa ina wachezaji wanne wanawake wanaosakata soka ughaibuni ambao ni Akida (Besiktas, Uturuki), kipa Annedy Kundu na beki Ruth Ingosi (Lakatamia, Cyprus) na kiungo Vivian Corazon Odhiambo Aquino (Atletico Ouriense, Ureno).