Habari Mseto

Msako Karatina wanasa washukiwa sita wa kuhangaisha abiria

May 9th, 2024 2 min read

NA MWANGI MUIRURI

MSAKO katika steji kuu ya Karatina mnamo Jumatano ulinasa washukiwa sita.

Hii ni baada ya wananchi kulalamika kwa maafisa wa usalama kuhusu genge la wanaume katika steji hiyo ambao hupiga, kutusi na kupora abiria.

“Mwendo wa saa tano asubuhi Jumatano, maafisa wa polisi walifika katika steji hiyo tukisaka washukiwa waliokuwa wameripotiwa kupora kutoka kwa abiria,” ripoti ya polisi yasema.

Mkuu wa polisi wa Mathira Mashariki Bw Benjamin Bunei alisema kwamba kati ya washukiwa hao sita, wawili ndio wameshatambuliwa na walalamishi.

Habari za kijasusi ambazo Taifa Leo imeona kuhusu kero ya magenge katika steji hiyo zinaelezea kwamba vijana hao walianza kujiunda mwaka wa 2019.

“Huwa wamejipenyeza katika steji hiyo na ambapo sio wahudumu halali. Kazi yao ni kushirikisha visa vya ujambazi. Miongoni mwa walalamishi ni hakimu mmoja wa Karatina ambaye mtoto wake aliporwa katika steji hiyo mwaka wa 2023,” ripoti hiyo yasema.

Wenyeji waliitaka serikali iwafurushe washukiwa wote wa genge hilo kutoka steji hiyo wakiteta wanawapa taswira ya utovu wa kiusalama na kuathiri biashara.

Waliteta kwamba licha ya jukumu la kudhibiti steji za uchukuzi kuwa la serikali za Kaunti, huwa zimuetelekeza na hivyo basi kuunda mazingara ya magenge kujipenyeza.

“Yale ambayo sisi hushuhudia kwa steji hii ya Karatina ni sawa na utundu ulio katika sera ya serikali. Hata Kuna Mzee mmoja mkongwe ambaye hutembea kwa kutumia mkongojo na huwa ni mporaji sugu. Lugha ya makanga huwa ni chafu huku hata kukiwa na abiria watoto,” akasema Bi Damacline Wagio.

Bi Wagio alisema utundu wa steji hiyo huchochewa sana na kuwepo kwa genge linalofungamanishwa na Mungiki, utumizi wa pombe na mihadarati pamoja na kujaa kwa madanguro ya ukahaba ambayo yako katika majengo mawili yaliyo mbele ya steji hiyo.

Bw Bunei alisema serikali haitavumilia magenge na ni lazima kupatikane suluhu ya kudumu.

Aliwaomba waathiriwa wawe wakipiga ripoti ili kuwahami maafisa wa polisi na uwezo wa kutekeleza misako.